Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania anatarajiwa kuzindua hospitali ya rufaa iliyopewa jina la Mwalimu Julius Kambarage Nyerere jijini Luanda, anapoanza ziara yake ya kikazi nchini Angola, Julai 31, 2026.
Kulingana na taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais ya Tanzania, Rais Samia anatarajia kushiriki hafla ya uzinduzi huo, akiwa na mwenyeji wake Joao Manuel Goncalves Lourenco.
Hafla hiyo ya uzinduzi, pia itahudhuriwa na Mama Maria Nyerere, mjane wa Mwalimu Nyerere.
Wakati huo huo, Rais Samia atafanya mazungumzo na mwenyeji wake pamoja na kushiriki hafla ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na Wake wa Marais wa Afrika, kwa lengo la kuchangisha fedha za utekelezaji wa shughuli za kijamii na kiuchumi za uwezeshaji wa wanawake na vijana.
Ziara hiyo ni mwendelezo wa kuimarisha uhusiano wa kihistoria na wa kindugu kati ya Tanzania na Angola, uliojengwa tangu enzi za harakati za ukombozi wa Bara la Afrika, kulingana na taarifa hiyo.















