Ajali ya mgodi wa dhahabu Sudan yasababisha vifo vya takriban watu 60

Mgodi wa dhahabu uliporomoka kusini mwa Sudan na kuua takriban wachimbaji wadogo 60, kulingana na maelezo ya manusura wawili kwa shirika la habari la AFP siku ya Jumatano, huku wengine wengi wakiwa hawajulikani walipo.

Newstimehub

Newstimehub

16 Septemba, 2026

2f4e7037 581a 4e5a ab65 e19b96420b3d 1789570373968

Takriban wachimbaji wadogo 60 wamefariki dunia baada ya mgodi wa dhahabu kuporomoka kusini mwa Sudan, idadi ya watu waliokwama chini ya ardhi bado haijulikani.

Kwa mujibu wa manusura wawili waliozungumza na shirika la habari la AFP Jumatano, sehemu za mgodi wa Al Zaraa, uliopo karibu na mji wa Al Nahud katika jimbo la Kordofan Magharibi, zilianza kuporomoka Jumanne. Kufikia Jumatano asubuhi, miili ya watu 60 ilikuwa tayari imetolewa kutoka kwenye mgodi huo.

Mmoja wa manusura hao, Khair Al Sayyed Jabara, amesema bado hawajui ni watu wangapi wamekwama chini ya ardhi.

“Hatujui ni wangapi bado wapo ndani,” amesema Jabara, akieleza kuwa operesheni ya uokoaji iliendelea usiku kucha ikifanywa na wachimbaji wenzao kwa kutumia zana wanazotumia katika shughuli zao za uchimbaji.

Amesema juhudi za uokoaji zinaendelea, lakini kazi hiyo imekuwa ngumu kutokana na miamba na udongo ulioporomoka.

“Kila mtu anafanya kazi kwa bidii kujaribu kutoa miili na kuokoa manusura, lakini ni vigumu. Tunahitaji mitambo mizito ili kuondoa miamba na udongo,” alisema.

Uchimbaji mdogo wa dhahabu waajiri zaidi ya watu milioni mbili

Uchimbaji wa dhahabu kwa njia za jadi na kwa kiwango kidogo ni sehemu kubwa ya uzalishaji wa dhahabu nchini Sudan. Shughuli hizo hufanyika katika migodi iliyokuwa imefungwa au maeneo yasiyo rasmi kama Al Zaraa.

Al Amin Suleiman, mchimbaji mwingine aliyekuwa akifanya kazi katika eneo la juu la mgodi huo Jumanne, alisema mashimo ya uchimbaji katika eneo hilo yako karibu sana.

“Mashimo yote hapa yako karibu karibu. Moja likiporomoka, husababisha yale yaliyo karibu nayo nayo yaporomoke,” alisema.

Suleiman amsema hali hiyo ndiyo iliyosababisha ajali hiyo na wakati akizungumza na AFP, miili 60 ilikuwa tayari imetolewa huku watu wengine wakiwa bado wamekwama chini ya ardhi tangu Jumanne.

Kwa mujibu wa takwimu za sekta hiyo, shughuli za uchimbaji wa dhahabu kwa njia za jadi na kwa kiwango kidogo huwaajiri zaidi ya watu milioni mbili nchini Sudan.

Sudan ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa dhahabu barani Afrika. Mwaka uliopita, nchi hiyo ilirekodi uzalishaji wa tani 70 za dhahabu, kiwango kilichoelezwa kuwa cha juu zaidi katika kipindi cha miaka mitano.

Hata hivyo, maafisa wa serikali wanasema sehemu kubwa ya dhahabu inayozalishwa nchini humo husafirishwa kwa njia za magendo nje ya nchi.