Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ametoa onyo kali dhidi ya uharibifu wa mali za umma, hususan miundombinu, akisisitiza kuwa serikali hutumia miaka mingi kutafuta fedha za kujenga na kuendeleza miradi hiyo.
Akizungumza, Rais Samia amesema: “Hatuwezi kutumia miaka mingi kutafuta fedha za kujenga miundombinu na kuanza kutoa huduma, halafu tukakubali juhudi hizo ziharibiwe ndani ya muda mfupi. Hili halikubaliki.”
Aidha, amewataka wananchi kushiriki kikamilifu katika kulinda mali za umma.
“Ninawaomba wananchi, ninyi wenyewe muwe walinzi wa mali hizi. Mtu anayeharibu mali za umma anateketeza kodi za wananchi. Anayefanya hivyo anachelewesha maendeleo ya taifa, analirudisha nyuma taifa, ni mhujumu wa taifa letu na ni adui wa taifa letu,” amesema.
Rais Samia alitoa kauli hiyo leo katika hafla ya uzinduzi wa miundombinu ya Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) Awamu ya Pili, iliyofanyika eneo la Temeke, Azizi Ali, mkoani Dar es Salaam.















