Watu zaidi ya 5,000 walioondolewa katika makazi yao kufuatia mashambulizi ya wapiganaji wa Sudan RSF wamewasili Damazin, mji mkuu wa jimbo la kusini mashariki la Blue Nile, huku hali kwa watu ikizidi kuwa mbaya, maafisa wa afya wa eneo hilo walisema siku ya Jumanne.
Katika taarifa, Mtandao wa Madaktari wa Sudan ulisema ulikuwa unafuatilia “kwa wasiwasi mkubwa” kuwasili kwa watu zaidi ya 5,000 ambao hivi karibuni waliondolewa katika makazi yao eneo la Geissan jimbo la Blue Nile kufuatia mashambulizi ya RSF.
Watu walioondolewa katika makazi yao, inasema, wanakabiliwa na uhaba wa chakula, dawa na tatizo la sehemu ya kuishi, kutishia hali za watu na hasa watoto, wanawake, na wazee.
Mtandao huo pia ulionya kuwa mvua kubwa katika jimbo la Blue Nile inaweza ikafanya hali kuwa mbaya zaidi kwa watu na kutatiza hali ya afya na mazingira kutokana na uchache wa raslimali.
Msaada wa chakula unahitajika
Katika taarifa, mtandao huo wa madaktari umetoa wito kwa Umoja wa Mataifa na mashirika ya misaada kusaidia watu walioondoka katika makazi yao na chakula, maji ya kunywa, dawa na mahema.
Pia walisisitiza umuhimu wa kuhakikisha kuwa msaada kwa watu unafikia walengwa haraka iwezekanavyo.
Siku ya Jumatatu, Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) limesema kuwa watu 5,355 – ikiwa ni familia zaidi 1,000 – wameondolewa katika makazi yao Geissan ndani ya kipindi cha kati ya Agosti 12 na 15 kutokana na ukosefu wa usalama.
Pia siku ya Jumatatu, mamlaka za eneo la Geissan zilisema kuwa jeshi la Sudan lilitibua mashambulizi katika eneo hilo, ambalo liko karibu na mpaka wa Ethiopia, lililokuwa limefanywa na wapiganaji wa RSF na SPLM-N.
Vita vibaya
Jeshi la Sudan linadhibiti sehemu kubwa ya jimbo la Blue Nile, ilhali SPLM-N imekuwa ikipigana dhidi ya serikali yenye makao yake mjini Khartoum tangu 2011, ikidai kuwa inataka mamlaka huru kwa Majimbo ya Sudan ya Kordofan Kusini na Blue Nile.
RSF na jeshi la Sudan wamekuwa wakipigana tangu 2023 chanzo ikiwa tofauti za ujumuishaji wa wapiganaji hao katika mfumo wa jeshi la taifa.
Vita hivi vinavyoendelea vimesababisha ukame na moja ya hali mbaya zaidi kwa watu na uchumi duniani.
Tangu wakati huo, vita hivyo vimesababisha vifo vya maelfu ya watu na kuwaondoa karibu milioni 13 wengine katika makazi yao, kulingana na makadirio.















