Tanzania kushuhudia punguzo la bei ya mafuta ifikapo mwezi Julai

Hali hiyo inatokana na kushuka kwa bei ya mafuta ghafi katika soko la dunia kufuatia kusitishwa kwa mapigano ya Mashariki ya Kati.

Newstimehub

Newstimehub

26 Juni, 2026

5ef92a1ed3182e8fc1631c5d115ed7e8e450a0d9ff7d420e2aa770e1a17e070d

Waziri wa Nishati nchini Tanzania Deogratius Ndejembi, amesema kuwa Watanzania wataanza kushuhudia kushuka kwa bei za mafuta kuanzia mwezi Julai mwaka huu.

Kulingana na Ndejembi, hali hiyo inatokana na kushuka kwa bei ya mafuta ghafi katika soko la dunia kufuatia kusitishwa kwa mapigano ya Mashariki ya Kati.

Akizungumza Bungeni jijini Dodoma, Juni 26, 2026, Ndejembi amesema kuwa, serikali ya Tanzania  imeanza kuzielekeza Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Wakala wa Ununuzi wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA) kuhakikisha manufaa ya kushuka kwa bei za mafuta yanawafikia walaji.

“Watanzania wataanza kuona punguzo la bei kuanzia mwezi Julai, na kadri shehena mpya za mafuta zilizonunuliwa kwa bei nafuu zitakavyoendelea kuwasili nchini, ndivyo bei zitakavyozidi kushuka,” alisema Ndejembi.

Alisema kuwa, licha ya vita kati ya Iran, Israel na Marekani kusababisha usumbufu katika usafirishaji wa mafuta kupitia Mlango wa Hormuz, Tanzania iliendelea kuwa na uhakika wa upatikanaji wa mafuta bila kukumbwa na uhaba.