Waziri wa Nishati nchini Tanzania Deogratius Ndejembi, amesema kuwa Watanzania wataanza kushuhudia kushuka kwa bei za mafuta kuanzia mwezi Julai mwaka huu.
Kulingana na Ndejembi, hali hiyo inatokana na kushuka kwa bei ya mafuta ghafi katika soko la dunia kufuatia kusitishwa kwa mapigano ya Mashariki ya Kati.
Akizungumza Bungeni jijini Dodoma, Juni 26, 2026, Ndejembi amesema kuwa, serikali ya Tanzania imeanza kuzielekeza Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Wakala wa Ununuzi wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA) kuhakikisha manufaa ya kushuka kwa bei za mafuta yanawafikia walaji.
“Watanzania wataanza kuona punguzo la bei kuanzia mwezi Julai, na kadri shehena mpya za mafuta zilizonunuliwa kwa bei nafuu zitakavyoendelea kuwasili nchini, ndivyo bei zitakavyozidi kushuka,” alisema Ndejembi.
Alisema kuwa, licha ya vita kati ya Iran, Israel na Marekani kusababisha usumbufu katika usafirishaji wa mafuta kupitia Mlango wa Hormuz, Tanzania iliendelea kuwa na uhakika wa upatikanaji wa mafuta bila kukumbwa na uhaba.















