Ufaransa, mataifa 25 yashtumu mauaji ya waandamanaji Iran

Taarifa ya pamoja inataka Iran kuachana na hukumu ya kifo na kuwaachia huru wale wote waliokamatwa bila hatia.

Newstimehub

Newstimehub

13 Agosti, 2026

29837333 99f8 44ad b1ae cd51131ebd75 1786614665365

Ufaransa na mataifa mengine 25 pamoja na Mkuu wa sera ya mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya siku ya Jumatano walishtumu “vikali” mauaji ya Iran kwa waandamanaji na kuendelea kutumia hukumu ya kifo.

“Kutumia hukumu ya kifo kunyamazisha wapinzani, kutishia jamii na kuwaadhibu watu binafsi kwa kutekeleza haki yao ya kimsingi haikubaliki,” walisema katika taarifa iliotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa.

Waliotia saini walisisitiza kuwa watu wa Iran wanatakiwa kuruhusiwa kutimiza haki yao ya uhuru wa kujieleza na mikusanyiko ya amani bila kuwa na hofu.

“Tunatoa wito kwa serikali ya Iran kuachana na hukumu ya kifo na kuwaachia huru wale wote waliokamatwa bila hatia,” ilisema.

Pia walitoa wito kwa Iran “kusikiliza sauti za watu,” ambao wanasema wanataka mabadiliko, na kuchukua hatua madhubuti ili kuhakikisha haki za binadamu zinaheshimiwa.

Taarifa hiyo ilitiwa saini na mataifa ikiwemo Ufaransa, Canada, Ujerumani, Australia, Denmark, Hispania, New Zealand, Uholanzi, Ureno, Sweden na Uingereza pamoja na Mkuu wa sera ya mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya Kaja Kallas.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi, kwa upande wake, alishtumu nchi hizo kwa unafiki kuhusu tarifa za haki za binadamu na sheria ya kimataifa.

“Nchi kama Ufaransa inatakiwa kuacha kutuambia kuhusu ‘haki za binadamu’ na sheria ya kimataifa. Unafiki wao ni wa wazi na unatia aibu.”

“Kuunga mkono mauaji ya halaiki ya Israel huko Gaza — na mashambulizi dhidi ya Iran — kumeharibu sifa yoyote ya maadili ambayo walikuwa wanadhani wanayo,” Araghchi alisema kwenye mtandao wa X.