Kampuni ya usafiri wa mtandao ya Uber imetangaza kusitisha shughuli zake nchini Nigeria na Uganda.
Mkurugenzi Mtendaji wa Uber, Dara Khosrowshahi, amesema hatua hiyo ni sehemu ya mpango wa kampuni wa kufanya marekebisho katika shughuli zake duniani baada ya kufanya tathmini ya biashara yake.
Kampuni hiyo yenye makao yake nchini Marekani, iliyoanzishwa mwaka 2009, iliingia katika soko la Nigeria—nchi yenye idadi kubwa zaidi ya watu barani Afrika—mwaka 2014. Ilianza katika jiji kubwa la Lagos kabla ya kupanua huduma zake katika maeneo mbalimbali nchini humo.
“Baada ya kufanya tathmini ya kina ya biashara yetu, tumefanya uamuzi mgumu wa kusitisha shughuli zetu nchini Nigeria kuanzia tarehe 2 Septemba 2026,” kampuni hiyo ilisema katika taarifa, bila kutoa maelezo zaidi.
Uber pia ilitangaza Jumatano kwamba inasitisha shughuli zake nchini Uganda. Kampuni hiyo iliondoka Tanzania mapema mwaka huu.
Marekebisho ya shughuli za Uber duniani
Kuondoka kwa Uber nchini Nigeria na Uganda kumetokea siku hiyo hiyo ambayo Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Dara Khosrowshahi, alitangaza kuwa Uber itapunguza asilimia 10 ya wafanyakazi wake duniani kote.
Hatua hiyo inatarajiwa kuathiri maisha ya madereva wa Nigeria waliokuwa wakitegemea jukwaa hilo kupata kipato, huku baadhi yao wakiwa tayari wanakabiliwa na athari za gharama kubwa za mafuta.
Wananchi wa Nigeria wamekuwa wakikabiliwa na hali ngumu ya gharama za maisha kufuatia mageuzi ya kiuchumi yaliyoanzishwa na Rais Bola Tinubu.
Wanauchumi na wawekezaji wameunga mkono hatua hizo, wakisema zimeongeza utulivu wa uchumi kwa ujumla. Hata hivyo, wakosoaji wanasema manufaa ya mageuzi hayo bado hayajawafikia wananchi wa kawaida.
Kutatua migogoro
Mwaka 2023, Meneja wa Uber nchini Nigeria, Tope Akinwunmi, alisema shughuli za kampuni hiyo zilikuwa zimechangia mabilioni ya naira (mamilioni ya Dola) katika uchumi wa nchi hiyo. Madereva wa Uber kwa pamoja walikuwa wakipata takribani naira bilioni 6.1 kwa mwaka.
Hata hivyo, madereva wa Uber wamekuwa wakilalamika kwa muda mrefu kwamba nauli zinazotozwa kupitia programu hiyo ni ndogo.
Uber imesema kituo chake cha msaada kwa wateja kitaendelea kupatikana hadi Septemba 23 ili kushughulikia na kutatua migogoro.
Kampuni shindani za usafiri kama vile Bolt na InDrive pia zinaendelea kufanya kazi nchini Nigeria.















