Mkosoaji wa serikali ya DRC akamatwa Tanzania

Mamlaka za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) zimesema kukamatwa kwa Denise Dusauchoy ni sehemu ya uchunguzi unaoendelea kuhusu tuhuma mbalimbali za uhalifu, na kwamba hatua hiyo haimaanishi kuwa amepatikana na hatia.

Newstimehub

Newstimehub

1 Septemba, 2026

cea8afd7 1e37 47cf 9e99 d8c1e75b82d2 1788252946156

Mwanahabari na mshawishi wa mitandao ya kijamii kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Denise Dusauchoy, alikamatwa mwishoni mwa wiki nchini Tanzania kwa ombi la mamlaka za DRC.

Katika taarifa iliyotolewa Jumatatu, Wizara ya Sheria ya DRC ilisema kukamatwa kwa Dusauchoy kulitokana na hati ya kukamatwa iliyotolewa na mahakama nchini humo.

Mamlaka nchini Congo, zimeeleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya uchunguzi unaoendelea kuhusu tuhuma kadhaa za uhalifu, na kusisitiza kuwa kukamatwa kwake hakumaanishi kuwa ana hatia.

Dusauchoy, ambaye amekuwa akiikosoa serikali ya Rais Félix Tshisekedi, pia amewahi kuonyesha hadharani kuunga mkono AFC/M23, muungano wa waasi unaodhibiti maeneo makubwa mashariki mwa DRC. Kundi hilo limekuwa katika mzozo wa kijeshi na jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Mnamo Disemba 2024, Dusauchoy alihukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela mjini Kinshasa kwa makosa ya kusambaza taarifa za uongo, kughushi nyaraka na kutoa matusi hadharani.