Marekani yasitisha huduma za viza katika miji 25 ya Afrika kuanzia Agosti 1, 2026

Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imetangaza kuwa itasitisha huduma za visa katika miji 25 barani Afrika.

Newstimehub

Newstimehub

30 Julai, 2026

227252f9 185a 4429 8c98 dda475e6d6e9 1785398353640

Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imetangaza kuwa itasitisha utoaji huduma wa viza katika miji 25 barani Afrika. Badala yake, huduma hizo zitahamishiwa kwenye vituo vya kikanda vilivyochaguliwa na serikali ya Marekani.

Katika taarifa iliyochapishwa Julai 15, Wizara ya Mambo ya Nje imesema kuwa, kuanzia Agosti 1, 2026, itafanya marekebisho ya utoaji wa huduma za viza katika miji hiyo.

Miji iliyoathirika ni:

Antananarivo (Madagascar), Abuja (Nigeria), Asmara (Eritrea), Bamako (Mali), Banjul (Gambia), Brazzaville (Jamhuri ya Congo), Bujumbura (Burundi), Conakry (Guinea), Cotonou (Benin), Durban (Afrika Kusini), Freetown (Sierra Leone), Gaborone (Botswana), Harare (Zimbabwe), Juba (Sudani Kusini), Libreville (Gabon), Lilongwe (Malawi), Lusaka (Zambia), Maputo (Msumbiji), Maseru (Lesotho), Mbabane (Eswatini), N’Djamena (Chad), Niamey (Niger), Nouakchott (Mauritania), Ouagadougou (Burkina Faso), na Windhoek (Namibia).

Waombaji viza ambao hapo awali walikuwa wakitarajia kushughulikia maombi yao ya viza katika balozi au ubalozi mdogo wa Marekani katika miji hiyo sasa watalazimika kusafiri kwenda miji mingine, au hata nchi nyingine, kwa ajili ya kupata miadi ya viza.

Kwa kuzingatia mwongozo wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, vituo vipya vya utoaji wa viza kwa waombaji kutoka miji hiyo ni kama ifuatavyo:

Antananarivo (Madagascar) — Johannesburg (Afrika Kusini)

Abuja (Nigeria) — Lagos (Nigeria)

Asmara (Eritrea) — Kampala (Uganda)

Bamako (Mali) — Dakar (Senegal)

Banjul (Gambia) — Dakar (Senegal)

Brazzaville (Jamhuri ya Congo) — Kinshasa (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo)

Bujumbura (Burundi) — Kampala (Uganda)

Conakry (Guinea) — Dakar (Senegal)

Cotonou (Benin) — Lomé (Togo)

Durban (Afrika Kusini) — Johannesburg (Afrika Kusini)

Freetown (Sierra Leone) — Monrovia (Liberia)

Gaborone (Botswana) — Johannesburg (Afrika Kusini)

Harare (Zimbabwe) — Johannesburg au Cape Town (Afrika Kusini)

Juba (Sudani Kusini) — Kampala (Uganda)

Libreville (Gabon) — Yaoundé (Cameroon)

Lilongwe (Malawi) — Nairobi (Kenya)

Lusaka (Zambia) — Johannesburg (Afrika Kusini)

Maputo (Msumbiji) — Johannesburg (Afrika Kusini)

Maseru (Lesotho) — Johannesburg (Afrika Kusini)

Mbabane (Eswatini) — Johannesburg (Afrika Kusini)

N’Djamena (Chad) — Yaoundé (Cameroon)

Niamey (Niger) — Lomé (Togo)

Nouakchott (Mauritania) — Dakar (Senegal)

Ouagadougou (Burkina Faso) — Lomé (Togo)

Windhoek (Namibia) — Johannesburg au Cape Town (Afrika Kusini)

Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imesema: “Raia na wakazi wa nchi hizi wanaotaka kuomba visa kuanzia Agosti 1, 2026, au baada ya tarehe hiyo, wanapaswa kupanga miadi na kulipa ada inayohitajika ya viza katika vituo vilivyochaguliwa vya kushughulukia viza zisizo za uhamiaji (Nonimmigrant Visa Locations) au vituo vilivyochaguliwa vya viza za uhamiaji (Immigrant Visa Locations).”

Majukumu mengine ya balozi na ubalozi mdogo yataendelea

Kuhusu aina za viza zitakazohamishiwa kwenye vituo hivyo vipya, Wizara ya Mambo ya Nje ilmeeleza kuwa mabadiliko hayo yanahusu huduma zote za viza, zikiwemo: Viza zisizo za uhamiaji (nonimmigrant visas), ikiwa ni pamoja na visa za utalii na biashara. Viza zisizo za uhamiaji zinazotolewa kwa msingi wa maombi yaliyowasilishwa (petition-based visas). Viza za uhamiaji kwa ndugu wa karibu, familia, viza zinazotokana na ajira, pamoja na viza za wachumba.

Hata hivyo, Marekani imesisitiza kuwa ingawa huduma za viza zimehamishwa kutoka katika maeneo hayo, hatua hiyo haimaanishi kuwa balozi au ofisi za ubalozi mdogo zimefungwa.

Majukumu mengine muhimu kwa niaba ya wananchi wa Marekani yataendelea kama kawaida.

Kwa mujibu wa Marekani, marekebisho hayo ya huduma za viza barani Afrika na katika maeneo mengine duniani ni sehemu ya utaratibu wa muda mrefu wa Wizara ya Mambo ya Nje unaolenga kuimarisha usalama wa taifa kupitia ulinganifu wa viwango vya uchunguzi, uhakiki na maamuzi ya maombi ya viza, pamoja na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.