Jiji la Dar es Salaam litakuwa mwenyeji wa Mkutano wa Infra for Africa Forum 2026 na Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa Africa50, utakaofanyika Agosti 5 hadi 6 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC).
Mkutano huo wa siku mbili unatarajiwa kuwakutanisha zaidi ya washiriki 1,000 wakiwemo wakuu wa nchi, mawaziri, wawekezaji, taasisi za fedha za maendeleo, viongozi wa sekta binafsi na wataalamu wa miundombinu kutoka Afrika na kwingineko.
Kulingana na waziri wa fedha wa Tanzania, Khamis Mussa Omar, maandalizi ya mkutano huo yanaendelea vizuri, huku ukitarajiwa kuvutia washiriki kutoka ndani na nje ya Afrika, wakiwemo viongozi wa Serikali, taasisi za fedha za kimataifa, wawekezaji, sekta binafsi na wadau wa maendeleo.
Alieleza kuwa mkutano huo unafanyika katika kipindi muhimu ambapo Africa50 inatimiza miaka kumi tangu kuanza rasmi shughuli zake mwaka 2016, taasisi iliyoanzishwa kwa ushirikiano kati ya Serikali za Afrika na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) ili kuharakisha utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya miundombinu barani Afrika.
“Tangu Tanzania ilipojiunga rasmi na Africa50 tarehe 14 Februari 2023 kama mwanahisa wa kundi la nchi za Afrika (African Sovereign States) imenufaika zaidi, hatua iliyopanua fursa za nchi kushiriki kikamilifu katika maandalizi, uendelezaji na ufadhili wa miradi mikubwa ya miundombinu” alisema waziri huyo.















