Maelfu ya watu wameandamana katika mji mkuu wa Niger siku ya Jumatano wakimuunga mkono kiongozi wa kijeshi wa taifa hilo la Afrika Magharibi, Jenerali Abdourahamane Tiani, na jeshi kufuatia kutibuliwa kwa uasi mwishoni mwa wiki, taarifa za vyombo vya habari zilisema.
Maandamano hayo mjini Niamey yamekuja siku chache baada ya wanaounga mkono serikali ya kijeshi kuzima jaribio la mapinduzi.
Miongoni mwa waliokuwepo katika mkusanyiko huo wa Jumatano ni maelfu ya raia wa Niger, ikiwemo mawaziri wa serikali.
Maandamano mengine kadhaa yalipangwa kufanyika katika miji mikubwa ya taifa hilo la Afrika magharibi, kulingana na vyombo rasmi vya habari.
“Tutaonesha dunia nzima kuwa watu wa Niger wako pamoja” na kwamba “uhaini hautovunja dhamira yetu”, waziri wa biashara Abdoulaye Seydou aliwaambia waandamanaji.
Mkuu wa Majeshi, Jenerali Amadou Ibro, pia alidai kuwa wafadhili wa waasi hao “wako nje ya nchi”.
Televisheni ya taifa imeshawahi kudai kuwa Ufaransa, Wakoloni wa zamani wa Niger, walikuwa wanachochea hali hiyo.
Kama ilivyo kwa serikali zingine za kijeshi jirani zao katika eneo la Sahel Burkina Faso na Mali, Niger pia imevunja uhusiano na Ufaransa.















