Tanzania yazindua ujenzi wa reli ya SGR Tabora hadi Kigoma

Kwa sasa, ujenzi huo umefikia zaidi ya asilimia 10, ukitegemewa kuzalisha jira 15,000 kwa wananchi wa Kigoma na Tabora.

Newstimehub

Newstimehub

20 Julai, 2026

06199b91 e6d5 46f8 8d6e 450cbd8f6f45 1784553837216

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania amezindua na kuweka jiwe la msingi kwenye awamu ya pili ya ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kwa kipande cha sita kutoka Tabora hadi Kigoma.

Mradi huo wenye urefu wa kilomita 506 unagharimu takribani dola za Marekani bilioni 2.74 na unalenga kuunganisha mkoa wa Kigoma na mikoa ya Tabora, Shinyanga, Mwanza, Dodoma, Morogoro na Dar es Salaam.

Aidha, reli hiyo itaimarisha usafirishaji wa mizigo na abiria kwa nchi jirani za Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na baadaye Zambia, huku ikiunganishwa na reli ya Uvinza Musongati nchini Burundi, hatua itakayoifanya Bandari ya Dar es Salaam kuwa lango muhimu la biashara kwa Ukanda wa Maziwa Makuu kupitia Central Corridor.

Mradi huo pia, unatarajiwa kupunguza muda wa safari kutoka Dar es Salaam kwenda Kigoma kutoka zaidi ya saa 20 za sasa hadi saa nane, huku ukanda wa Magharibi ukitarajiwa kufunguliwa kiuchumi.

Kwa sasa, ujenzi huo umefikia zaidi ya asilimia 10, ukitegemewa kuzalisha jira 15,000 kwa wananchi wa Kigoma na Tabora.