Mwigulu Nchemba awataka Watanzania kuweka akiba ya kutosha ya chakula

Ushauri wa Waziri Mkuu huyo wa Tanzania unakuja wakati maeneo tofauti ya nchi hiyo yakishuhudia kuchelewa kwa mvua.

Newstimehub

Newstimehub

15 Desemba, 2025

cb5d0dc76ebe5bfeb7cafd5378faa145b5cd9c16eb15038201e969145323c12f

Waziri Mkuu wa Tanzania, Mwigulu Nchemba amewataka Watanzania watunze akiba ya chakula walichonacho na waepuke matumizi yasiyofaa kutokana na hali ya kuchelewa kwa msimu wa mvua.

Akizungumza na baadhi ya Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya, ofisini kwake Mlimwa, jijini Dodoma, Nchemba alisema kuwa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilitoa utabiri wa mwelekeo wa msimu wa mvua za vuli na mvua za msimu kwa kipindi cha Oktoba 2025 hadi Disemba 2025 na kipindi cha mwezi Novemba, 2025 hadi Aprili 2026 mtawalia.

“Kutokana na utabiri huo, baadhi ya mikoa nchini inatarajiwa kuwa na mvua za chini ya wastani hadi wastani na kutawaliwa na vipindi virefu vya ukavu na mtawanyiko wa mvua usioridhisha,” amesema.

Kulingana na Nchemba, TMA ilionesha hali ya kuchelewa kwa mvua inatarajiwa katika maeneo ya mikoa ya Dodoma, Katavi, Kigoma, Singida, Tabora, Iringa, Mbeya, Mtwara, Njombe, Songwe, Rukwa, Ruvuma pamoja na Kusini mwa Mkoa wa Morogoro.

“Pamoja na kuwa hakuna tishio la uhaba wa chakula kutokana na hifadhi ya chakula iliyopo nchini, lakini ni vema, wananchi waendelee kuzingatia matumizi sahihi ya chakula. Tuna akiba ya chakula ya kutosha lakini ninawasihi wananchi waweke akiba na kuepuka matumizi yasiyo ya lazima,” alisisitiza.

Kiongozi huyo alitumia fursa hiyo kuwakumbusha wakulima nchini Tanzania, kuandaa mashamba kwa wakati na watumie pembejeo zinazoendana na upatikanaji wa mvua chache sanjari na kuzingatia ushauri wa wataalamu wa kilimo ambao kwa sasa wanazunguka nchi nzima kukutana na wakulima, wakitoa elimu.