Serikali ya Ghana imekubali mapendekezo ya kuongeza muda wa muhula wa urais kutoka miaka minne hadi mitano, waziri wa sheria wa taifa hilo la Afrika Magharibi alisema siku ya Alhamisi.
Rais John Dramani Mahama aliunda kamati mwaka uliopita ambayo iliangalia upya katiba ya mwaka 1992 na kuwasilisha mapendekezo, baadhi ambayo yamekubaliwa na serikali.
Mwanasheria Mkuu na Waziri wa Katiba Dominic Awine anasema muda wa bunge pia utaongezwa kwenda sanjari na muhula wa urais.
Kuongeza muda ni kwa lengo la kuwapa viongozi nafasi ya kutosha kuongoza, serikali ilisema.
Umri wa chini kugombea kubadilishwa
“Miezi ya kwanza ya kila serikali inakuwa zaidi ni kipindi cha mpito, na mwaka wa mwisho unakuwa wa uchaguzi.” Awine alisema.
Serikali imekubali kimsingi mapendekezo ya kamati ya kushusha umri wa wagombea urais, ambao kwa sasa ni 40, lakini wakaweka 35 badala ya 30 uliokuwa umependekezwa na kamati.
Serikali pia imekubali kuwa uchaguzi wa urais ufanyike kila wiki ya kwanza ya mwezi Novemba kuhakikisha kuna muda wa kutosha kati ya upigaji kura na Januari 7 ambayo ni siku ya kuapishwa.
Kamati nyingine itaanzishwa kuandika miswada miwili inayotarajiwa kuwa tayari kufikia Oktoba 2026.
Muswada unaotathmini muda wa urais inabidi upitie hatua kadhaa kabla ya kura ya maoni 2027.
Ili kura ya maoni ipite, inabidi watu wajitokeze kupiga kura ikiwa ni 40% ya waliojisajili, huku watu wasiopungua 75% wakitarajiwa kuunga mkono mapendekezo hayo.















