Rais wa Marekani Donald Trump ametishia kuchukua hatua ya kijeshi dhidi ya Oman kama itaingilia kati majadiliano kati ya Marekani na Iran, huku akisema kuwa wanafanya mazungumzo ya moja kwa moja na kikosi cha Iran cha IRGC.
“Kama Oman itakwamisha mazungumzo, tutaishambulia kwa mabomu,” Trump aliiambia Fox News siku ya Jumatatu kuhusu hatua yake kwenye majadiliano yanayohusisha Iran na Mlangobahari wa Hormuz.
Iran ilisema siku ya Jumamosi kuwa imefikia makubaliano na Oman kuhusu ramani ya njia ya bahari ya Mlangobahari wa Hormuz kufuatia wiki kadhaa za kuanza mazungumzo.
Kuhusu Iran, Trump alisema nchi hiyo inatakiwa “kujisalimisha,” akiongeza: “Wanajua kucheza mchezo, lakini wanakufa.”
Pia alithibitisha kuwa Marekani inawasiliana kwa njia isiyo rasmi na IRGC.
“Tunawasiliana na IRGC kwa njia isio rasmi. Tunazungumza moja kwa moja na maafisa wa IRGC nchini Iran,” Trump alisema.
Mashambulizi ya Israel Gaza
Kuhusu Gaza, alisema: “Israel haitakiwi kushambulia Gaza. Hamas imekubali kusalimisha silaha zake.”
Trump pia alisema kuwa Marekani inaendelea na njia zingine za kuwasiliana na Hamas.
“Tuna njia nyingine za mawasiliano na Hamas, na hatimaye wanasalimisha silaha zao,” alisema.
Matamshi hayo yanakuja huku Marekani ikiendeleza juhudi za kutekeleza mpango wa Trump wa amani Gaza, ambao unajumuisha kuwapokonya silaha Hamas na jeshi la Israel kuondoka katika eneo hilo.
Alipoulizwa kuhusu siasa za Israel, Trump alisema anaamini kuwa “hatua sahihi” ni kwa yeye kutojihusisha na uchaguzi wa nchi hiyo, huku akieleza uwezekano wa kumuunga mkono mgombea.
“Nadhani ni hatua sahihi kwa mimi kutoingilia uchaguzi huo wa Israel, lakini naweza kumuunga mtu mkono,” alisema.















