Polisi nchini Afrika Kusini wanasema wanachunguza kifo cha raia wa kigeni aliyeuawa na kundi la watu karibu 50 katika mji wa Durban.
Polisi walisema katika mtandao wa X kuwa aliyeuawa alikuwa kati ya umri wa miaka 30 na 40, na alipigwa na watu na kuuawa papo hapo.
Kundi hilo la watu lilikuwa likiandamana katikati mwa mji wa Durban wakati watu wawili walipoondoka na kumkabili mtu huyo, ambapo alishambuliwa na watu karibu 50, polisi walisema siku ya Alhamisi.
Polisi hawakueleza uraia wa aliyeuawa na kusema kuwa sababu ya kuuawa kwake pia haijafahamika.
Tukio hilo linafuata maandamano ya miezi kadhaa dhidi ya wahamiaji nchini Afrika Kusini, ambayo baadhi yao yamekuwa na vurugu, kusababisha maelfu ya wahamiaji kutoka nchi za Kiafrika kuondoka katika maeneo yaliyokuwa yanashambuliwa.
Mapema mwezi huu, biashara zinazomilikiwa na raia wa kigeni ziliporwa na magari kuchomwa wakati wa maandamano dhidi ya wahamiaji mjini Durban na mtaa wa Soweto jijini Johannesburg baada ya maandamano ya kupinga kupokelewa kwa maombi ya wanaoomba hifadhi katika kituo cha kuwapokea wakimbizi.















