Siku ya Ijumaa Saudi Arabia imetangaza kukamilika salama kwa ibada ya Hajj ya mwaka huu, ikisema kuwa mifumo iliyoimarishwa ya usalama, ushirikiano na utoaji huduma’ iliwawezesha mahujaji kukamilisha ibada hiyo bila usumbufu na kwa amani.
Tangazo hizo lilitolewa na Mwanamfalme Saud bin Mishal bin Abdulaziz, naibu gavana wa Makkah na naibu mwenyekiti wa Kamati ya Hajj na Umrah, katika taarifa iliotangazwa kupitia televiseheni usiku wa kukamilika kwa ibada hiyo ya kila mwaka.
Mwanamfalme Saud anasema Hajj ya mwaka huu 2026/1447 AH imekuwa na “mifumo iliyoimarishwa ya usalama, ushirikiano na utoaji huduma” ambayo ilitoa fursa kwa mahujaji kukamilisha ibada hiyo bila usumbufu na kwa usalama.
Saud alisisitiza kuwa mafanikio ya Hajj hayaashirii mwisho wa kazi lakini mwanzo wa majukumu mengine, akisisitiza dhamira ya Saudi Arabia ya kila mwaka ya kuendeleza jukumu lake la kutoa huduma kwa Uislamu na Waislamu.
Siku ya Jumanne, Mamlaka ya Takwimu ya Saudi Arabia ilisema idadi ya mahujaji mwaka huu ilikuwa 1,707,301, ikiwemo mahujaji 1,546,655 kutoka nje ya Saudia Arabia wakiwakilisha mataifa 165. Mahujaji wengine 160,646 walitimiza ibada hiyo ya Hajj wakitokea ndani ya Saudi Arabia.
Idadi hii ni zaidi ya mwaka uliopita ya 1,673,230 kwa mahujaji kutoka ndani na nje ya Saudi Arabia lakini bado ni ndogo ikilinganishwa na zaidi ya milioni 1.83 ya 2024. Ibada hiyo ya kila mwaka inakamilika siku ya Jumamosi.
Ibada ya Hajj ilianza rasmi siku ya Jumatatu huku mahujaji wakiwasili Mina, magharibi mwa Saudi Arabia, na huduma zimeimarishwa pamoja na hatua za usalama kwa lengo la kuwapa mahujaji unafuu wa kukamilisha ibada hiyo.
Ibada hiyo ya siku sita ya Hajj imejumuisha kisimamo cha Arafat siku ya Jumanne, kuwepo usiku kucha Muzdalifah, ishara ya kumpiga shetani mawe, na kutufu katika Mskitini Mkubwa Makkah.














