Mtoto wa Rais Museveni Muhoozi Kainerugaba atangaza nia ya kugombea 2031

Muhoozi Kainerugaba anasema kuwa anatarajia kushinda kwa kishindo katika uchaguzi wa 2031, kulingana na ujumbe katika mtandao wa X.

Newstimehub

Newstimehub

26 Agosti, 2026

35da99c2 9ac4 4921 85b3 76774bc40ccc 1787752877456

Mkuu wa Majeshi wa Uganda Muhoozi Kainerugaba, ambaye pia ni mtoto wa Rais wa nchi hiyo Yoweri Museveni, anasema kuwa atagombea Urais mwaka 2031.

Kainerugaba, 52, mara nyingi ametajwa kuwa mrithi wa baba yake.

“Nitagombea wadhifa wa juu nchini mwaka 2031. Na tutashinda kwa uwezo wa Mungu,” Kainerugaba alisema katika moja ya ujumbe wake kwenye mtandao wa X siku ya Jumanne.

“Nikiwa na baba yangu mpendwa, Mzee akiniunga mkono nitapata 90% ya kura katika uchaguzi wa mwaka 2031,” aliongeza kwa kumsifia baba yake mwenye umri wa miaka 81.

Kainerugaba, ambaye anaongoza vuguvugu la kisiasa linaloitwa ‘Patriotic League of Uganda’, aliwahi kutangaza kuwa angegombea katika uchaguzi uliopita mwezi Januari lakini hakutimiza hilo.

Muhula wa saba

Museveni, ambaye anaongoza chama tawala cha National Resistance Movement, amekuwa kiongozi wa Uganda tangu 1986. Alishinda muhula wa saba katika uchaguzi uliofanyika Januari 2026.

Kiongozi wa upinzani nchini humo, Bobi Wine, alikwenda uhamishoni nchini Marekani mapema mwaka huu, akisema kuwa anahofia usalama wake. Mwanasiasa mwingine wa upinzani, Kizza Besigye, amekuwa gerezani tangu 2024 na anakabiliwa na kesi ya uhaini.

Alipoulizwa kama Museveni atagombea muhula mwingine, msemaji wa serikali Alan Kasujja aliiambia Reuters, “kama ilivyokuwa miaka iliopita, Rais Museveni na chama anachokiongoza wataamua pale wakati utakapofika.”