Liberia yamshtaki aliyekuwa Makamu wa Rais, kwa tuhuma za dawa za kulevya

Mamlaka pia zimewafungulia mashitaka watu watatu wanaodaiwa kuwa wanachama wa mtandao huo — raia wawili wa Croatia na raia mmoja wa Ukraine, licha ya kuwa raia hawo hawapo nchini Liberia.

Newstimehub

Newstimehub

20 Agosti, 2026

33a3a7c8 4672 4bfc 84ab 1e1fbfe974b0 1787219176740 main

Liberia imemfungulia mashitaka aliyekuwa Makamu wa Rais, Jewel Howard-Taylor, kwa makosa ya kusafirisha dawa za kulevya, utakatishaji fedha na makosa mengine, ikiwa ni sehemu ya uchunguzi dhidi ya mtandao wa kimataifa wa biashara ya dawa za kulevya, Mwanasheria Mkuu wa nchi hiyo ya Afrika Magharibi alisema katika taarifa Jumatano.

Kukamatwa kwa Howard-Taylor, ambaye ni mke wa zamani wa Charles Taylor, aliyepatikana na hatia ya uhalifu wa kivita, kumekuja siku kadhaa baada ya mamlaka za Liberia kutangaza kukamata kokeini yenye thamani ya takriban Dola milioni 317 iliyokuwa ikisafirishwa kuelekea Ulaya. Tukio hilo limeangazia kuongezeka kwa nafasi ya Liberia katika biashara ya dawa za kulevya duniani.

“Hakutakuwa na upendeleo katika suala la kushitakiwa, ulinzi wa kisiasa, watu wasioguswa na sheria, wala maridhiano na uhalifu uliopangwa,” taarifa hiyo ilisema.

“Kila mtu ambaye ushahidi wa kuaminika na unaokubalika kisheria utaonekana dhidi yake atachunguzwa na kushtakiwa bila hofu, upendeleo au kuzingatia masuala ya kisiasa.”

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Howard-Taylor alizuiwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Roberts alipokuwa akijaribu kuondoka nchini na kisha kupelekwa katika makao makuu ya polisi wa kitaifa.

Mashitaka dhidi yake pia yanajumuisha kuingiza nchini bila kibali dawa inayodhibitiwa kisheria, kushawishi kutendwa kwa uhalifu na kupiga njama ya kutenda uhalifu, taarifa hiyo ilisema.

Wakili wa Howard-Taylor, Kabineh M. Ja’neh, aliliambia Shirika la Habari la Reuters kwamba alikutana na mteja wake Jumatano na kwamba mamlaka zilimweleza kuwa zilikuwa na nia ya kumfungulia mashitaka, ingawa bado hakuwa ameona hati rasmi ya mashitaka.

“Yuko chini ya ulinzi wa Polisi wa Liberia usiku huu. Atalala huko,” alisema.

“Tutaweza kuanza kushughulikia suala hili mara tutakapopata mashitaka rasmi.”

Mamlaka pia zimewafungulia mashitaka watu watatu wanaodaiwa kuwa wanachama wa mtandao huo — raia wawili wa Croatia na raia mmoja wa Ukraine, licha ya kuwa raia hawo hawapo nchini Liberia.

Taarifa hiyo imesema serikali itaanzisha mchakato wa kukamatwa kwao kupitia njia za kisheria za ndani na kimataifa.

Howard-Taylor alikuwa Makamu wa Rais chini ya Rais wa zamani George Weah kuanzia Januari 2018 hadi Januari 2024.