Mtu tajiri zaidi barani Afrika raia wa Nigeria Aliko Dangote na Rais wa Kenya William Ruto wataweka jiwe la msingi siku ya Jumatano kwa ajili ya kuanza kwa ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta cha gharama ya $16 bilioni kwa lengo la kukabiliana na hitaji kubwa la bidhaa za petroli kote Afrika Mashariki.
Dangote anataka kuwa na kiwanda kama cha Nigeria ambapo kitasafisha mapipa 700,000 kwa siku huku nchi zikiwemo Kenya na Uganda zikijiandaa kuzalisha mafuta ghafi.
Kiwanda hicho cha Kenya kinatarajiwa kukamilika mwaka 2030, kikiwa na lengo la kupunguza gharama za bei ya mafuta katika eneo hilo na kuokoa fedha za kigeni wanazotumia kuagiza bidhaa zilizosafishwa.
“Unapoangalia Afrika Mashariki, siyo Afrika Mashariki pekee, nyingi ya nchi hizo 54 barani Afrika, zinaagiza bidhaa za petroli,” Dangote aliwaambia waandishi wa habari jijini Nairobi siku ya Jumanne.
Kujitosheleza
“Tunachojaribu kufanya ni kuhakikisha kuwa tunajitosheleza kwa kile tunachotumia.”
Dangote amependekeza hisa za jumla ya 30% kwa serikali za eneo hilo za kiwanda hicho cha kusafisha mafuta.
Matumizi ya kila mwaka ya bidhaa za petroli katika eneo hilo yanakadiriwa kuwa kati ya tani milioni 20 na milioni 30, anasema David Ndii, mshauri mwandamizi wa uchumi wa Rais Ruto.
Ili kukabiliana na hitaji hilo kiwanda kinabidi kiwe na uwezo wa kusafisha mapipa zaidi ya milioni 1 kwa siku, kulingana na mtaalamu wa masuala ya fedha anayehusika na viwanda vya mafuta barani Afrika.
Eneo hilo limekabiliwa na gharama kubwa za bei ya mafura kutokana na vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran, kusababisha maandamano hatari kwa mataifa kama Kenya kutokana na bei kubwa ya mafuta. .















