Seneta wa Kakamega Boni Khalwale anaomboleza kifo cha mkewe, Gloria Sekeiyan Khalwale, aliyefariki ghafla asubuhi ya Jumamosi baada ya kupatwa na mshtuko wa moyo.
Khalwale alitangaza kifo cha Gloria katika ukurasa wa X mnamo Agosti 15, akisema alianguka ghafla na kufariki kufuatia mshtuko huo wa moyo.
Gloria alikuwa mama wa watoto wanane wa Khalwale.
Kifo chake kimeibua ujumbe wa rambirambi kutoka kwa viongozi wa kisiasa na wananchi, huku Maseneta wenzake wakionyesha mshikamano na seneta huyo pamoja na familia yake.
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa chama cha ODM, Philip Etale, alielezea kifo cha Gloria kuwa cha ghafla na kutoa rambirambi kwa Khalwale, familia yake, jamii ya Malinya huko Ikolomani na Kaunti nzima ya Kakamega.
Kifo cha Gloria kinakuja takriban miaka saba baada ya Khalwale kumpoteza mkewe wa kwanza, Adelaide Shikanga, aliyefariki mnamo Oktoba 2019.
Adelaide alikuwa akipambana na saratani ya shingo ya kizazi tangu mwaka 2003 na baadaye aligunduliwa kuwa na saratani ya damu ‘multiple myeloma.’ Khalwale alisema alikuwa ametangazwa kupona saratani hiyo ya damu baada ya matibabu kabla ya kupatwa na tatizo la shinikizo la juu la damu kwenye mishipa ya mapafu muda mfupi kabla ya kifo chake.















