Tanzania na Uganda zimetia saini makubaliano na kampuni ya kimataifa ya biashara ya bidhaa za petroli, Vitol, ili kukiendeleza mji wa bandari wa Tanga nchini Tanzania kuwa kituo cha kikanda cha nishati; mradi ambao unaweza kuvutia uwekezaji wa zaidi ya dola bilioni 20 za Marekani.
Hati ya Makubaliano ilitiwa saini jijini Dar es Salaam na Shirika la Taifa la Mafuta la Uganda (UNOC), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Vitol Bahrain, huku ikishuhudiwa na Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan na mwenzake wa Uganda, Yoweri Museveni.
Kituo hicho kinachopendekezwa kinatarajiwa kuhusisha miundombinu ya kuhifadhi na kusafisha mafuta, biashara na usambazaji wa mafuta, pamoja na mabomba na vifaa vingine vya mafuta na gesi. Mradi huu unajengwa juu ya ushirikiano wa nishati uliopo kati ya nchi hizo mbili, hasa mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki lenye urefu wa kilomita 1,443, linalounganisha visima vya mafuta vya Uganda na bandari ya Tanga.
Tanzania inasema mpango huu unalenga kuiondoa kanda hiyo katika hatua ya kusafirisha mafuta ghafi pekee na kuelekea kwenye kuongeza thamani zaidi, viwanda na usalama wa nishati.
Kwa upande wa Uganda, ambayo inajiandaa kuanza uzalishaji wa mafuta kibiashara, Tanga inatoa njia muhimu ya kufikia masoko ya kimataifa na kituo kinachoweza kutumika kusambaza mafuta katika kanda hiyo.
Makubaliano hayo hayana vipengele vya kisheria vinavyolazimisha utekelezaji wa moja kwa moja; hii ina maana kuwa uwekezaji na miundombinu inayopendekezwa bado itahitaji tafiti zaidi, makubaliano na ufadhili kabla ya ujenzi kuanza.
Hata hivyo, serikali hizo mbili zinasema ushirikiano huo unaweza kuifanya Tanga kuwa kituo kikubwa cha nishati na biashara kinachohudumia Tanzania, Uganda na masoko mengine kote Afrika Mashariki.















