Tanzania kukutanisha wadau watakaojadili changamoto za Mto Nile

Jukwaa hilo litawakutanisha serikali, watunga sera, watafiti, sekta binafsi, mashirika ya kiraia na washirika wa maendeleo kujadili usimamizi wa pamoja wa maji, uhifadhi wa mazingira na maendeleo endelevu.

Newstimehub

Newstimehub

7 Agosti, 2026

62d4c4b5 19c3 4456 9218 fde2da8818bb 1786107128869

Wakati mabadiliko ya tabianchi, uharibifu wa mazingira na mahitaji ya maji yakiongeza na shinikizo katika Bonde la Mto Nile, Tanzania sasa imeanza maandalizi ya jukwaa la kimataifa litakalowakutanisha wadau kutoka nchi zinazohusishwa na bonde hilo kujadili mustakabali wa rasilimali hiyo muhimu.

Hatua hii ni sehemu moja wapo ya kukabiliana na changamoto kama hizo. Nchi hiyo itakuwa mwenyeji wa Jukwaa la Nane la Maendeleo ya Bonde la Mto Nile (Nile Basin Development Forum – NBDF), linalotarajiwa kufanyika Novemba 25–27 mwaka huu.

Jukwaa hilo litawakutanisha serikali, watunga sera, watafiti, sekta binafsi, mashirika ya kiraia na washirika wa maendeleo kujadili usimamizi wa pamoja wa maji, uhifadhi wa mazingira na maendeleo endelevu.

Kando ya uzinduzi wa maandalizi ya jukwaa hilo uliofanyika Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, aliwaambia waandishi wa habari kuwa mustakabali wa Bonde la Mto Nile hauwezi kulindwa na nchi moja.

“Hakuna nchi inayoweza kulinda Bonde la Mto Nile peke yake. Ushirikiano wa kikanda ndiyo njia pekee ya kuhakikisha rasilimali hii inaendelea kuwa salama na kunufaisha vizazi vya sasa na vijavyo.”

Mwajuma amesema jukwaa hilo litatoa nafasi ya kutafuta suluhisho ya pamoja, na pia linalenga kutafuta kiasi cha fedha kitakachosaidia kulindwa.

Bonde hilo linakabiliwa na changamoto lukuki ikiwemo uharibifu wa vyanzo vya maji, ukataji miti, matumizi holela ya kemikali katika kilimo na athari za mabadiliko ya tabianchi.

“Tunaendelea kukata miti bila kupanda mingine. Hii ni changamoto kubwa kwa mustakabali wa Bonde la Mto Nile,” amesema Mwajuma.

Hata hivyo, katika uzinduzi huo, Wizara ya Maji imezindua tovuti rasmi ya Nile Basin Development Forum, inayowawezesha watafiti, waandishi wa habari na wadau wengine kujisajili na kushiriki katika mijadala na tafiti.

Pia kutakuwa na mashindano ya uandishi wa habari yatakayolenga kuongeza uelewa wa umma kuhusu umuhimu wa Bonde la Mto Nile na namna ya kulilinda.

Mto unaobeba maisha ya mamilioni

Mkurugenzi Mtendaji wa Nile Basin Initiative (NBI), Mhandisi Nestor Niyonzima, amesema Mto Nile una nafasi kubwa katika maisha na uchumi wa watu wanaoishi katika nchi zinazolizunguka bonde hilo.

“Mto Nile si chanzo cha maji pekee, bali ni msingi wa maisha ya mamilioni ya watu. Kuulinda kunahitaji ushirikiano wa kisayansi, kisera na kifedha kati ya nchi wanachama.”

Bonde hilo linahusisha Tanzania, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Misri, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Sudan Kusini, Sudan na Uganda, huku Eritrea ikishiriki katika baadhi ya mifumo ya ushirikiano.

Mto huo una umuhimu mkubwa katika kilimo, usalama wa chakula, uzalishaji wa nishati na shughuli za kiuchumi katika eneo hilo.

Jukwaa hilo linatarajiwa kujadili usimamizi wa pamoja wa rasilimali za Bonde la Mto Nile, mabadiliko ya tabianchi, ulinzi wa vyanzo vya maji na uwekezaji.

Kwa nchi zinazotegemea bonde hilo, mjadala huu unaenda zaidi ya maji. Unahusu maisha, chakula, nishati, mazingira na mustakabali wa mamilioni ya watu.

Macho yote sasa yataelekezwa Tanzania itakapowakutanisha wadau wa Bonde la Mto Nile kutafuta majibu ya swali moja tu. 

Je, ushirikiano wa kikanda unaweza kuhakikisha Mto Nile unabaki kuwa chanzo cha maisha na maendeleo kwa vizazi vijavyo?