Bunge la Uganda limeidhinisha kupelekwa kwa wanajeshi wake Gaza kama sehemu ya Kikosi cha Kimataifa cha Kuleta Utulivu kilichopendekezwa na Baraza la Amani la Rais wa Marekani Donald Trump, kwa lengo la kuhakikisha usalama katika eneo hilo baada ya vita vilivyosababisha uharibifu mkubwa kati ya Israel na Hamas.
Hoja hiyo, iliyowasilishwa na Waziri wa Ulinzi, ilipitishwa na Bunge na kuwa ishara ya kwanza ya wazi kwamba Uganda iko tayari kushiriki katika Kikosi cha Kimataifa cha Kuleta Utulivu Gaza. Morocco nayo tayari imeahidi kuchangia wanajeshi wake kwa ajili ya operesheni hiyo.
Hadi sasa hakuna ufafanuzi wowote ni kwa nini Uganda imekubali kupeleka wanajeshi Gaza, wala kama kulikuwa na makubaliano ya kubadilishan maslahi yaliyofikiwa.
Baadhi ya wabunge wa upinzani walitilia shaka sababu za Uganda kufanya uamuzi huo.
Mbunge Hassan Kirumira alisema hatua hiyo inaweza kuzua “hofu za kidiplomasia” kwa kuwa Uganda ni mwanachama wa Shirika la Ushirikiano wa Kiislamu (OIC).
Akiwa bungeni, Kirumira aliuliza swali kwa wanaounga mkono uamuzi huo akisema: “Jeshi letu litakuwa linapigana upande gani?”
Waziri wa Ulinzi, Kiryowa Kiwanuka, akiomba uungwaji mkono wa wabunge, alisema Uganda ina uwezo wa kijeshi uliotokana na uzoefu wake katika misheni za kulinda amani katika nchi mbalimbali, ikiwemo Somalia.
Kikosi hicho kilipendekezwa na Baraza la Amani la Trump mwezi Februari, na kinatarajiwa kuongozwa na Meja Jenerali wa Marekani Jasper Jeffers. Jeffers alisema mwezi Mei kwamba kikosi hicho chenye wanajeshi takribani 20,000 kitasaidia kuhakikisha “ustawi wa baadaye na amani ya kudumu.”
Wiki iliyopita, Trump alitangaza kufikiwa kwa makubaliano ya Hamas kuweka chini silaha na Israel kuondoa majeshi yake kutoka Gaza.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo, Kikosi cha Kimataifa cha Kuleta Utulivu kingepelekwa Gaza baada ya kukamilika kwa uondoaji wa hatua kwa hatua wa majeshi ya Israel.
Makubaliano hayo, ambayo ni sehemu ya mpango mpana wa usitishaji mapigano uliofikiwa mwaka uliopita, yanaitaka Israel kusitisha operesheni zake za kijeshi na Hamas pamoja na washirika wake Gaza kusimamisha shughuli zote za kijeshi.















