Jeshi la Nigeria limekanusha taarifa zinazodai kuwa raia waliuawa wakati wa mashambulizi ya angani katika eneo la Shiroro, Jimbo la Niger, likisisitiza kuwa operesheni hiyo ililenga majambazi na kusababisha vifo vya wapiganaji kadhaa.
Katika taarifa siku ya Jumapili, Mkurugenzi wa Jeshi wa Masuala ya Habari, Meja Jenerali Michael Onoja, alisema mashambulizi yalianzishwa baada ya taarifa za kijasusi kuonesha kuwa majambazi walikuwa wamekusanyika katika Kijiji cha Lukupe eneo la Shiroro Mei 9, 2026.
Kulingana na Makao Makuu ya Jeshi, droni za jeshi la Nigeria zilifanya mashambulizi ya angani kati ya saa tano na dakika hamsini na tisa usiku Mei 10 na saa kumi na mbili asubuhi, zikilenga maficho ya majambazi maeneo ya vijiji vya Katerma, Bokko, Kusasu na Kuduru.
Onoja anasema taarifa za kijasusi zilizopatikana kutoka kwa vyanzo vya maeneo hayo zinaonesha kuwa mashambulizi hayo “yalikuwa mahsusi” katika vijiji vya Kusasu, Katerma na Bokko, kukanusha madai kuwa raia waliuawa.
Kukabiliana na ukosefu wa usalama
Alieleza kuwa majambazi karibu 70 wameuawa katika kijiji cha Kusasu pekee, huku wapiganaji walionusurika wakionekana kuondoa miili ya wenzao kwa ajili ya kwenda kuzika.
“Kwa mujibu wa majukumu ya Jeshi la Nigeria la kufanya operesheni ya kumaliza ukosefu wa usalama kote nchini, taarifa za kijasusi zilionesha majambazi wamekusanyika katika kijiji cha Lukupe huko Shiroro,” taarifa hiyo ilisema.
“Wakati huo huo, Kitengo cha Jeshi la Nigeria cha droni, kufuatia taarifa za kijasusi, kilifanya mashambulizi kadhaa ya angani katika maeneo mbalimbali ya makundi hayo, ikiwemo vijiji vya Katerma, Bokko, Kusasu na Kuduru. Taarifa zaidi kutoka kwa vyanzo vya eneo hilo zimethibitisha kuwa mashambulizi hayo yalilenga maeneo mahsusi yaliyokusudiwa.”
Mashambulizi ya angani ya jeshi la Nigeria dhidi ya makundi yenye silaha yametegemea zaidi droni katika maeneo ya vijijini ambapo makundi hayo yenye silaha yako kwenye misitu na sehemu zisizofikika kwa urahisi. Hata hivyo, mashambulizi ya angani ya siku zilizopita yamezua utata kufuatia matukio ya raia kuuawa kimakosa katika mashambulizi hayo.














