Tanzania yatoa wito wa amani Gaza

Akihutubia Kikao cha 81 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Makamu wa Rais wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, amesema Tanzania inaendelea kusisitiza umuhimu wa kupatikana kwa suluhisho la kudumu kwa mgogoro kati ya Israel na Palestina.

Newstimehub

Newstimehub

23 Septemba, 2026

a73de331 03ae 42fd 81c7 d4d4981f5be9 1790151684642

Tanzania imetoa wito wa kulindwa kwa raia, kuruhusiwa kwa msaada wa kibinadamu bila vikwazo na kuhuishwa kwa diplomasia yenye lengo la kupata amani ya kudumu katika ukanda wa Gaza na Mashariki ya Kati.

Akihutubia Kikao cha 81 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Septemba 22, 2026, Makamu wa Rais wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, amesema Tanzania inaendelea kusisitiza umuhimu wa kupatikana kwa suluhisho la kudumu kwa mgogoro wa Israel na Palestina.

Ndejembi ameongeza kwa kusema kuwa, Tanzania inaunga mkono suluhisho la nchi mbili, ambapo Israel na Palestina zitaishi pamoja kwa amani na usalama, kwa kuzingatia sheria za kimataifa na maazimio husika ya Umoja wa Mataifa.

Vilevile amesema Tanzania inatambua haki ya watu wa Palestina ya kujitawala na kwamba amani ya kudumu inapaswa kuzingatia utu, usalama na matarajio halali ya pande zote mbili.

“Msimamo huo umekuwa sehemu ya sera ya Tanzania ya mambo ya nje kwa miongo kadhaa,” alisema Ndejembi.

Katika hotuba yake, Ndejembi alielezea msimamo wa Tanzania kuhusu umuhimu wa kuheshimu mamlaka ya nchi na sheria za kimataifa, huku ikipinga hatua za upande mmoja zinazoweza kuathiri uchumi na ustawi wa wananchi wa nchi zinazolengwa.

Vilevile ameeleza kuwa, Tanzania inaunga mkono ushirikiano wa kimataifa unaozingatia mamlaka ya kila nchi na kuhimiza kuondolewa kwa hatua zinazoweka vikwazo katika maendeleo na utekelezaji kamili wa haki za binadamu.

Akizungumzia nafasi ya Umoja wa Mataifa katika masuala ya amani, amesema migogoro inayoendelea duniani inaonesha umuhimu wa kuimarisha mfumo wa kimataifa unaozingatia Mkataba wa Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa.

Amesisitiza kuwa Umoja wa Mataifa unapaswa kuendelea kuwa jukwaa la haki, mshikamano na maendeleo, huku nchi wanachama zikiheshimu misingi ya Mkataba wake katika kujenga mustakabali salama kwa wote.