Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Emmanuel Nchimbi, ametembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Uwanja wa Arusha unaojengwa jijini Arusha, ambao unatarajiwa kutumika katika Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.
Akizungumza baada ya ukaguzi huo, Nchimbi amepongeza kasi na maendeleo ya ujenzi wa uwanja huo, akisema ni jambo la faraja kuona ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwezesha Tanzania kuwa mwenyeji wa michuano hiyo ikitekelezwa kwa vitendo.
Aidha, Makamu wa Rais huyo, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha zinazowezesha utekelezaji wa mradi huo na kuhakikisha unakamilika kwa wakati.
Pia ameipongeza Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, uongozi wa Mkoa wa Arusha, wakandarasi pamoja na mshauri elekezi kwa kazi kubwa wanayoifanya katika ujenzi wa uwanja huo.
Hali kadhalika, Nchimbi amewataka viongozi wa wizara husika na Mkoa wa Arusha kuhakikisha wanasimamia ipasavyo utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kukamilisha kwa wakati barabara zote zinazorahisisha upatikanaji wa uwanja huo.















