Tanzania kuendelea kuimarisha ushirikiano wa forodha kikanda – Kamishna Mkuu wa TRA

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Juma Mwenda, amesema Tanzania itaendelea kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika masuala ya forodha ili kuongeza ufanisi wa biashara na kulinda uchumi wa nchi.

Newstimehub

Newstimehub

14 Mei, 2026

f386c8143e2c132e910f758621c67a296e0317bac31b58eb369bad5df2661913

Yusuph Juma Mwenda ameyasema hayo wakati wa Mkutano wa 32 wa Baraza la Uongozi la Shirika la Forodha Duniani Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika (WCO ESA) uliofanyika leo Mei 14, 2026 katika Ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip, Zanzibar.

Akizungumza katika mkutano huo, Kamishna Mkuu Mwenda amesema Tanzania imeendelea kuwa lango muhimu la biashara na kitovu cha kuaminika kwa wawekezaji na washirika wa kimataifa, akieleza kuwa mabadiliko ya biashara ya dunia yanayochochewa na teknolojia, biashara za mtandaoni na akili mnemba (AI) yanahitaji mifumo imara ya forodha yenye uwezo wa kurahisisha biashara na kulinda uchumi wa nchi.

Aidha, ameeleza kuwa TRA imepiga hatua kubwa katika mageuzi ya kidijitali kupitia Mfumo wa Elektroniki wa Ushirikiano wa Forodha Tanzania, ambao umeboresha uwazi, kasi ya huduma na uratibu wa taasisi mbalimbali katika mnyororo wa biashara.

Mwenda pia amesisitiza kuwa licha ya maendeleo hayo, bado kuna umuhimu wa kuendelea kuimarisha uwezo wa kiusalama mipakani kwa kutumia teknolojia za kisasa kama mashine za ‘skana za kukagua mizigo, ndege zisizo na rubani (drones) na mifumo ya ufuatiliaji wa hatari ili kudhibiti magendo na biashara haramu.

Kwa mujibu wa Kamishna Mkuu Mwenda, majadiliano hayo ni fursa muhimu ya kuimarisha mshikamano wa kikanda na kuboresha utendaji wa taasisi za forodha ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa jamii katika ukanda wa ESA na dunia kwa ujumla.