Shinikizo linaongezeka kwa serikali ya Sudan Kusini kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha uchaguzi wa Disemba 2026 unafanyika kwa haki na uwazi, kufuatia wasiwasi ulioibuliwa kuhusu hali ya usalama na mvutano wa kisiasa.
Baada ya tahadhari zilizotolewa na wachambuzi na wadau wa kisiasa, mashirika ya kiraia pamoja na jumuiya ya kimataifa sasa yanaitaka serikali kuimarisha usalama hasa katika maeneo yenye migogoro kama jimbo la Jonglei.
Wadau hao wanaeleza kuwa bila mazingira salama, uchaguzi huo unaweza kukosa uhalali na kusababisha kurejea kwa migogoro iliyoshuhudiwa kabla ya mkataba wa amani wa 2018.
Pia, suala la kukamatwa kwa Makamu wa Kwanza wa Rais, Riek Machar, linaendelea kutajwa kama kikwazo kikubwa kwa maridhiano ya kisiasa. Baadhi wanasisitiza umuhimu wa mazungumzo ya kisiasa ili kupunguza mvutano kabla ya uchaguzi kufanyika.
Licha ya ahadi ya serikali kuwa uchaguzi hautaahirishwa tena, wadau wanasisitiza kuwa mafanikio ya mchakato huo yatategemea sana hatua zitakazochukuliwa sasa kuhakikisha usalama, ushirikishwaji na uwazi.
CHANZO: Newstimetr














