Ushirikiano wa Uturuki na Pakistan katika sekta ya nishati umeingia katika hatua mpya kufuatia kuwasili kwa meli ya utafiti ya Uturuki, Oruc Reis, katika Bandari ya Karachi nchini Pakistan.
Akizungumza katika hafla ya kuipokea meli hiyo siku ya Alhamisi, Waziri wa Nishati wa Uturuki, Alparslan Bayraktar, alisema nchi hizo mbili zilitia saini mikataba kadhaa ya ushirikiano katika sekta ya nishati mjini Islamabad mwaka jana.
Mikataba hiyo iliweka msingi wa ushirikiano kati ya Shirika la Mafuta la Uturuki (TPAO) na kampuni za kitaifa za nishati za Pakistan ambazo ni OGDCL, PPL na Mari Energies.
Bayraktar alisema ushirikiano huo ni hatua muhimu katika kuimarisha uhusiano wa kihistoria kati ya mataifa hayo mawili.
“Sisi ni mataifa mawili yenye historia inayojengwa katika misingi ya maadili ya pamoja na undugu wa muda mrefu. Leo, tumekutana kuchukua hatua ya kihistoria itakayoimarisha zaidi urafiki wetu na kuunda mustakabali wa sekta ya nishati ya nchi zetu mbili,” alisema.
Oruc Reis kuanza utafiti wa mafuta na gesi
Bayraktar alisema taratibu za utoaji wa leseni kwa ajili ya vitalu vitano vya utafutaji wa mafuta na gesi zimekamilika. Vitalu hivyo vinajumuisha maeneo matatu ya baharini na mawili ya nchi kavu, huku shughuli za utafiti zikiwa zimeanza.
Alisema meli ya Oruc Reis iliwasili Pakistan baada ya safari ya siku 19 na imepewa jukumu la kufanya utafiti katika mabonde ya Indus na Makran ili kubaini uwezekano wa kuwepo kwa akiba ya mafuta na gesi.
Kwa mujibu wa Bayraktar, Oruc Reis kwa kushirikiana na Shirika la Mafuta la Uturuki (TPAO), itafanya vipimo vya kijiolojia vya pande tatu (3D seismic surveys) katika eneo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 670 ndani ya kitalu cha Indus-C.
Shughuli hizo zinatarajiwa kuchukua takribani miezi miwili.
“Kwa kutegemea taarifa tutakazokusanya, tunalenga kuanza shughuli za uchimbaji katika maeneo yatakayobainishwa mwaka ujao,” alisema Bayraktar.
Aliongeza kuwa shughuli hizo za utafiti zinaweza kuchangia maendeleo na kuimarisha usalama wa upatikanaji wa nishati katika nchi zote mbili.
Uturuki kushirikisha Pakistan uzoefu wa kutafuta mafuta na gesi
Bayraktar alisema Uturuki inalenga kuleta nchini Pakistan mafanikio ambayo imeyapata katika shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi ndani ya nchi yake.
Aliashiria ugunduzi wa akiba kubwa ya gesi asilia katika Bahari Nyeusi mwaka 2020, ambao aliuelezea kuwa ugunduzi mkubwa zaidi wa gesi asilia katika maeneo ya baharini duniani kwa mwaka huo.
Alisema kwa sasa Uturuki inazalisha takribani mita za ujazo milioni 10 za gesi asilia kwa siku kutoka katika maeneo hayo, kiasi kinachokidhi mahitaji ya takribani kaya milioni nne.
Kwa mujibu wa waziri huyo, uzalishaji unatarajiwa kuongezeka hadi kufikia takribani mita za ujazo milioni 40 kwa siku ifikapo mwaka 2028, kiasi kitakachoweza kuhudumia takribani kaya milioni 16.
“Tunatoa uzoefu na uwezo wa kihandisi tulioupata kupitia shughuli hizi ili kuwanufaisha ndugu na dada zetu wa Pakistan,” alisema.
Bayraktar aliongeza kuwa Uturuki na Pakistan zina fursa kubwa za kuimarisha ushirikiano katika sekta za nishati, umeme na madini, akibainisha kuwa mikataba mipya itasaidia kuimarisha zaidi ushirikiano huo.
Mikataba ya pamoja ya utafutaji wa madini yasainiwa
Katika hatua nyingine, Wizara ya Nishati ya Uturuki ilitangaza kusainiwa kwa mikataba miwili ya ubia kati ya MTAIC, taasisi iliyoanzishwa kupitia ushirikiano wa Kurugenzi Kuu ya Utafiti na Uchunguzi wa Madini ya Uturuki (MTA) na kampuni ya ETI Maden, pamoja na kampuni ya Mari Energies Minerals ya Pakistan na Shirika la Maendeleo ya Madini la Pakistan (PMDC).
Chini ya makubaliano hayo, MTAIC itaanza shughuli za utafutaji wa madini katika maeneo matatu nchini Pakistan. Maeneo mawili yatahusu utafutaji wa shaba na dhahabu, huku eneo jingine likilenga madini ya elementi ya kikemikali ya stibi.
Aidha, hati tofauti ya makubaliano (MoU) ilisainiwa kati ya MTA, MTAIC na Taasisi ya Jiolojia ya Pakistan.
Makubaliano hayo yanalenga kuimarisha kushirikishana taalamu na uzoefu katika masuala ya jiolojia na utafutaji wa madini, pamoja na kuwezesha utekelezaji wa miradi ya pamoja.















