Shirika la Umeme la Sudan linasema mashambulizi ya droni ya wapiganaji wa RSF yameharibu mitambo ya kufua umeme, na kusababisha kukatika kwa huduma hiyo kote kusini mashariki mwa nchi.
Mashambulizi hayo yalilenga vituo vya Singa, Al-Hawata, Al-Faw, Mashkur na Al-Junaid katikati na kusini mashariki mwa Sudan, shirika hilo lilisema kwenye taarifa siku ya Jumatatu.
“Mashambulizi yamesababisha uharibifu mkubwa kwa maeneo hayo na kufanya umeme kukatika kutoka kwa gridi ya kusini mashariki, kuathiri majimbo ya Sennar, Gedaref, White Nile na Gezira,” ilisema taarifa hiyo ikinukuu vyombo vya habari vya eneo hilo.
Ilionya kuwa uharibifu huo pia unatatiza gridi ya umeme ya taifa la Sudan.
‘‘Wahandisi na mafundi wamepelekwa katika maeneo yaliyoathirika kutathmini uharibifu na kuanza ukarabati kwa lengo la kurudisha umeme na kuweka sawa gridi mara moja,” iliongeza.
Maeneo ya kuhifadhi mafuta hatarini
Gazeti la The daily Sudan Tribune lilisema kuwa droni za RSF zilishambulia kituo cha umeme cha Al-Junaid mashariki mwa jimbo la Gezira mapema siku ya Jumatatu, kutatiza huduma na kusababisha kukatika kwa umeme eneo hilo.
RSF imezidisha mashambulizi ya droni katika siku za hivi karibuni yakilenga maeneo ya kuhifadhi mafuta na miundombinu ya umeme katika majimbo ya Kordofan Kaskazini, Gedaref, Gezira na White Nile huku mapigano yakizidi kati yao na Jeshi la Sudan.















