Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini amewaomba viongozi wa Jumuia ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) kushirikiana katika kukabiliana na tatizo la wahamiaji wanaoingia nchini humo, baada ya kuibuka kwa maandamano dhidi ya raia wa kigeni na kusababisha maelfu ya wahamiaji kuondoka nchini humo.
Rais Ramaphosa amesema katika hotuba yake Jumatatu akiwa mjini Durban kwamba Afrika Kusini imewasilisha taarifa kuhusu “changamoto ya uhamiaji” kwa viongozi wa Jumuiya hiyo ambapo alieleza masikitiko yake kuhusu yaliyotokea nchini humo.
Maandamano yaliyodumu kwa wiki kadhaa, yaliyoongozwa na makundi yenye msimamo mikali yaliyotaka raia wa kigeni wasio na nyaraka halali kuondoka nchini humo ifikapo Juni 30.
Maandamano hayo yalisababisha zaidi ya watu 176,000 kuondoka katika wiki za hivi karibuni, kwa mujibu wa idadi iliotolewa na Shirika la Habari la AFP zilizotokana na takwimu za serikali za nchi husika.
Afrika Kusini imewasilisha taarifa kuhusu “changamoto ya uhamiaji” kwa viongozi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), amesema Ramaphosa katika hotuba yake ya kufunga mkutano huo uliofanyika katika mji wa pwani wa Durban.
“Tumetoa shukrani kwa nchi za ukanda wetu kwa kuelewa changamoto tulizokabiliana nazo na ambazo bado tunaendelea kukabiliana nazo,” amesema kiongozi huyo wa Afrika Kusini.
“Pia tulieleza masikitiko yetu kuhusu yaliyotupata kama nchi. Tulieleza nia yetu kwamba sote tushirikiane katika kukabiliana na changamoto ya uhamiaji,” aliongeza.
Afrika Kusini, ambayo ni taifa lenye uchumi mkubwa zaidi barani Afrika, kwa muda mrefu imekuwa kivutio kwa wahamiaji. Hata hivyo, nchi hiyo inakabiliwa na kiwango cha ukosefu wa ajira kinachozidi asilimia 30 pamoja na ukosefu mkubwa wa usawa wa kiuchumi.
Mapema Jumatatu, takribani waandamanaji 300 wanaopinga uhamiaji waliandamana kuelekea eneo la mkutano huo, wakidai viongozi waliokusanyika “waje kuwachukua watu wao”.
Helikopta na ndege zisizo na rubani zilionekana kuruka juu ya eneo hilo, huku maafisa wa polisi waliokuwa wamepanda farasi na pikipiki wakiusimamia umati huo uliokuwa mdogo na kuupeleka hadi kwenye uzio wa eneo la mkutano.
“Tuko hapa kuwaambia waje kuwachukua watu wao ambao wako hapa Afrika Kusini kinyume cha sheria,” alisema kiongozi wa maandamano hayo, Jacinta Ngobese-Zuma, ambaye ni miongoni mwa watu waliohusishwa na wimbi la hivi karibuni la maandamano.
Alitaja Malawi, Msumbiji na Zimbabwe, ambazo raia wake ni sehemu kubwa ya maelfu ya raia wa kigeni walioondoka Afrika Kusini.
Baadhi yao waliondoka kwa hiari, huku wengine wakifukuzwa nchini au kusaidiwa kuondoka kupitia mipango ya serikali ya kuwarejesha katika nchi zao.
Katika mhadhara wa umma siku ya Ijumaa, uliofanyika kando ya mkutano wa SADC, Ramaphosa alisema Afrika Kusini “imekuwa na wasiwasi mkubwa na inaona aibu” kwamba raia wa nchi nyingine wamekuwa wakikabiliwa na ubaguzi na kutendewa vibaya katika miezi ya hivi karibuni.
Kwa mujibu wa polisi wa Afrika Kusini, angalau wahamiaji wanne waliuawa katika ghasia hizo, ingawa baadhi ya serikali za kigeni zimesema idadi ya waliofariki ni kubwa zaidi.
Namna serikali ilivyoshughulikia maandamano na ghasia hizo imekosolewa na nchi nyingine za Afrika, hususan Ghana na Nigeria, ambazo si wanachama wa SADC.
Afrika Kusini, ambayo imechukua uenyekiti wa zamu wa SADC katika mkutano huo, imetoa wito wa kufanyika kwa mkutano wa bara zima la Afrika ili kujadili na kushughulikia suala la uhamiaji.















