Bingwa wa mbio za marathoni, afungiwa miaka mitatu kwa matumizi ya dawa zilizopigwa marufuku

Shirikisho la Riadha linlosimamia masuala ya Uadilifu (AIU) limethibitisha kuwa Peres Jepchirchir amepigwa marufuku kushiriki mashindano kwa kipindi cha miaka mitatu, kuanzia Oktoba 20.

Newstimehub

Newstimehub

19 Novemba, 2026

61f16cfe 4e25 4e51 9b98 a929563e536e 1795083502178

Bingwa mtetezi wa dunia wa mbio za marathoni, Peres Jepchirchir, amefungiwa kwa miaka mitatu kwa kutumia dawa zinzosisimua misuli. Shirikisho la Riadha linalosimamia masuala ya Uadilifu (AIU) limetangaza uamuzi huo siku ya Alhamisi, ikiwa ni pigo jingine kwa sifa na hadhi ya riadha ya Kenya.

Jepchirchir, mwenye umri wa miaka 33, ni mwanariadha mwenye mafanikio makubwa, alitwaa medali ya dhahabu katika michezo ya Olimpiki ya Tokyo mwaka 2021.

Alisimamishwa kushiriki mashindano baada ya sampuli ya vipimo kubaini uwepo wa chembechembe za EPO, dawa inayosisimua misuli.

AIU imethibitisha kuwa adhabu yake ya kutoshiriki mashindano ni miaka mitatu, kuanzia Oktoba 20.

Wanariadha wengine wawili kutoka Kenya pia wamepigwa marufuku.

Veronica Loleo, aliyeshinda medali ya fedha katika mbio za nusu marathoni kwenye Mashindano ya Dunia ya Mbio za mwaka 2026, amefungiwa kwa miaka mitatu kwa kosa hilo hilo.

Naye Ronald Korir, aliyemaliza katika nafasi ya nne kwenye Mbio za Marathoni za Berlin mwaka 2023, amefungiwa kwa miaka sita baada ya kushindwa kutoa maelezo kuhusu dosari zilizobainika katika vipimo vya mfululizo vinavyofuatilia mabadiliko ya viashiria vya kibaolojia vya mwanariadha (Athlete Biological Passport).

Idadi ya wanariadha wa Kenya waliofungiwa yaendelea kuongezeka

Idadi ya wanariadha kutoka Kenya imefikia140, akiwemo anayeshikilia rekodi ya dunia ya mbio za marathoni kwa wanawake, Ruth Chepngetich, ambaye amesimamishwa au kupigwa marufuku na AIU tangu mwaka 2017.

Katika taarifa yake, Mkurugenzi Mtendaji wa AIU, Brett Clothier, alisema: “Serikali ya Kenya imepiga hatua kubwa katika mapambano dhidi ya matumizi ya dawa zilizopigwa marufuku katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Hata hivyo, visa hivi vinaonyesha kuwa bado kuna safari ndefu ya kufikia lengo hilo.”

Aliongeza kuwa serikali ya Kenya inafahamu hali ilivyo sasa na imeahidi kuimarisha zaidi Shirika la Kupambana na Matumizi ya Dawa Zilizopigwa Marufuku nchini Kenya (ADAK), pamoja na kuchukua hatua dhidi ya mitandao ya kihalifu inayorahisisha vitendo hivyo nchini humo.

AIU ilisema kuwa sampuli ya Jepchirchir ilichukuliwa nchini Kenya wakati ambapo hakuwa akishiriki mashindano, kabla ya ushindi wake katika Mbio za Marathoni za Sydney mwezi Agosti.

Aliwahi kushikilia rekodi ya dunia

Katika historia yake ya mafanikio, Jepchirchir pia aliwahi kushikilia rekodi ya dunia ya mbio za nusu marathoni. Aidha, ameshinda mara nne katika mashindano makubwa ya marathoni duniani (World Marathon Majors).

Mafanikio yake hayo yanajumuisha ushindi katika Mbio za Marathoni za London mwaka 2024, Boston mwaka 2022 na New York mwaka 2021.

Uamuzi wa Shirikisho la Riadha Duniani (World Athletics) kuipa Nairobi, Kenya, nafasi ya kuandaa Mashindano ya Dunia ya Riadha mwaka 2029 huenda ukaongeza ufuatiliaji wa sera na juhudi za nchi hiyo katika kupambana na matumizi ya dawa zilizopigwa marufuku michezoni.

Mwezi uliopita, Kenya ilipokea ujumbe wa Shirika la Dunia la Kupambana na Matumizi ya Dawa Zilizopigwa Marufuku (WADA) kwa ziara ya siku tatu.

Mkuu wa WADA, Witold Banka, aliiambia Kenya kuwa inapaswa kujitahidi kuhakikisha inakabiliana na matumizi ya dawa hizo.

“Kenya inajivunia kuitwa Nchi ya Mabingwa. Hata hivyo, ili nchi hiyo iendelee kuheshimiwa na kuaminika, ni lazima pia ihakikishe kuwa michezo yake hayakiuki sheria,” alisema Banka.