Bunge la Uturuki limeuidhinisha Mkataba wa Pamoja wa Ulinzi wa Makkah, kati ya Uturuki, Saudi Arabia na Pakistan, hatua inayofungua uwezekano wa Uturuki kutoa msaada wa kijeshi kwa Saudi Arabia wakati nchi hiyo ikiendelea kukabiliwa na mashambulizi ya wapiganaji wa kundi la Houthi kutoka Yemen.
Chini ya makubaliano hayo, ambayo yaliidhinishwa na wabunge mapema Ijumaa, shambulizi dhidi ya nchi moja mwanachama litachukuliwa kuwa ni shambulizi dhidi ya wanachama wote.
Akizungumzia mkataba huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje ya Bunge la Uturuki, Fuat Oktay, amesisitiza kuwa ushirikiano huo umejikita katika kujilinda na wala si kupanga mashambulizi dhidi ya mataifa mengine.
Mkataba huo ulipitishwa kwa kura 279, dhidi ya 119, katika Bunge lenye jumla ya viti 600.
Makubaliano hayo yalitiwa saini Agosti 7 katika mji mtakatifu wa Makkah, Saudi Arabia, na Mwanamfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman, Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan pamoja na Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif.
Kupitia mkataba huo, viongozi hao walikubaliana kuimarisha usalama wa pamoja, kupanua ushirikiano wa kijeshi na kuendeleza amani na utulivu katika eneo hilo na maeneo mengine duniani.
Kwa mujibu wa waraka wa makubaliano hayo, nchi nyingine za ukanda huo zinaweza kujiunga na ushirikiano huo iwapo ziko tayari kuchangia juhudi za kuimarisha amani, utulivu na usalama, huku zikiheshimu sheria za kimataifa, mipaka ya nchi, uhuru wa mipaka ya mataifa na kanuni ya kutokuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine.
Oktay amesema kuwa Uturuki haitaruhusu kuingizwa katika mchakato usiodhibitika kinyume na matakwa yake. Ameongeza kuwa hatua yoyote ya kupeleka wanajeshi katika nchi nyingine itahitaji kwanza kupata idhini ya Bunge kupitia utaratibu mwingine wa baadaye.
Makao makuu ya sekretarieti kuwa Riyadh
Mawaziri kutoka nchi hizo tatu tayari wamekutana mara mbili, katika miji ya Istanbul na Riyadh. Wakati huohuo, ujumbe wa ngazi za juu kutoka mataifa hayo ulifanya mazungumzo mjini Tehran, nchini Iran mwezi uliopita, katika juhudi za kuzuia kurejea kwa mapigano mapya yanayohusiana na vita vya Marekani dhidi ya Iran.
Kwa mujibu wa mkataba huo, sekretarieti ya ushirikiano huo itakuwa na makao yake makuu nchini Saudi Arabia.
Jenerali mstaafu wa Pakistan, Nauman Mahmood, ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa kwanza wa muungano huo, kwa kipindi cha miaka mitatu.
Mkataba huo utaendelea kwa kipindi cha miaka 10. Baada ya muda huo, nchi mwanachama itakayotaka kujiondoa italazimika kutoa taarifa ya miezi mitatu kabla ya kujitoa rasmi.















