Rais wa Marekani, Donald Trump, ameamua kwa sasa kutotoa amri ya kufanya mashambulizi dhidi ya kundi la Wa-Houthi nchini Yemen, licha ya ombi la Saudi Arabia kutaka Marekani iingilie vita hivyo. Hayo yameripotiwa na gazeti la The New York Times (NYT), likiwanukuu maafisa wa serikali ya Marekani.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Mwanamfalme wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman, alimpigia Trump simu siku ya Alhamisi kwa mara nyingine kutaka Marekani kuchukua hatua za kijeshi, wakati mapigano yalipokuwa yakiongezeka.
Trump, ambaye siku moja kabla alikuwa amewaambia washauri wake kwamba hakuwa akiunga mkono mashambulizi hayo, baadaye aliiagiza Pentagon kujiandaa kwa uwezekano wa mashambulizi ya anga.
Hata hivyo, kufikia Jumapili, Trump alikuwa ameamua kutofanya mashambulizi hayo kwa sasa, gazeti hilo liliripoti.
Majadiliano hayo yanafanyika wakati Marekani ikitaka ushirikiano wa Saudi Arabia katika mzozo wake na Iran, huku pia ikijaribu kuepuka kufungua uwanja mwingine wa mapigano katika eneo hilo.
Afisa mmoja mwandamizi wa serikali ya Marekani aliliambia gazeti hilo kwamba Marekani ina mkataba wa ulinzi na Saudi Arabia na kwamba “daima tutawalinda washirika wetu.”















