Vyama vya upinzani nchini Kenya vimetoa wito kwa Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kuchukua hatua dhidi ya Rais wa Kenya William Ruto, kufuatia ghasia za hivi karibuni za kisiasa zilizoshuhudiwa katika maeneo mbalimbali nchini Kenya.
Katika taarifa iliyosomwa kwa niaba ya upinzani, Kiongozi wa chama cha People’s Liberation Party (PLP), Martha Karua, ameangazia mashambulizi ya hivi karibuni dhidi ya wanasiasa wa upinzani wakati wa mikutano ya hadhara hivyo kuitaka serikali kueleza jinsi vurugu hizo zilivyoweza kutokea chini ya uangalizi wake.
Karua amesema ICC inapaswa kuangalia upya mashtaka yaliyowahi kuwasilishwa dhidi ya Rais Ruto na kutathmini iwapo kesi hiyo inapaswa kufunguliwa tena.
“Tunatoa wito kwa mwendesha mashtaka wa ICC kufuatilia kwa karibu matukio yanayoendelea nchini Kenya na kutathmini iwapo taarifa za kuaminika zinatoa msingi wa kuanzisha uchunguzi,” alisema.
“Iwapo ushahidi utajitokeza kwamba mashambulizi yaliyoenea au ya kimfumo dhidi ya raia yanaandaliwa, kugharamiwa, kuelekezwa au kufimbiwa macho na watu walio katika mamlaka, tunataka mwendesha mashtaka amchunguze Rais Ruto, ambaye aliwahi kufikishwa ICC, na kutathmini upya mashtaka yaliyowahi kuwasilishwa dhidi yake.”
Kiongozi huyo wa PLP aliwahimiza wananchi kukataa ghasia za kisiasa kwa aina zake zote, ikiwa ni pamoja na kuenea kwa vitendo vya kihuni vinavyofanywa na magenge.
“Ulinzi wa demokrasia hauwezi kuachwa kwa wananchi na viongozi wa kisiasa pekee; ni jukumu la kila Mkenya. Kwa hivyo, tunawataka Wakenya wote kukataa ghasia za kisiasa kwa aina zake zote, bila kujali ni nani anayezitekeleza au ni nani anayesema atanufaika nazo,” aliongeza.
“Hakuna mwananchi anayepaswa kunyimwa haki ya kufanya kampeni, kukusanyika au kupiga kura kwa sababu wanamgambo wenye silaha wameachiliwa dhidi yao. Uchaguzi wa 2027 lazima uwe mashindano ya sera na mawazo, si ya vitisho; mashindano ya kura, si ya risasi.”
Mwaka 2013, ICC ilimshtaki Rais Ruto kwa mashtaka matatu ya uhalifu dhidi ya binadamu, kuhusiana na ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007/08.
Miaka mitatu baadaye, mahakama hiyo ya The Hague ilifunga kesi hiyo, ikitaja ukosefu wa ushahidi wa kutosha. Hata hivyo, ICC ilisema kesi hiyo inaweza kufunguliwa upya iwapo ushahidi zaidi utapatikana.















