Rais wa Marekani, Donald Trump, amepuuza pingamizi la Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, kuhusu uwezekano wa Marekani kuiuzia Uturuki ndege za kivita aina ya F-35.
Akizungumza na waandishi wa habari akiwa ndani ya ndege ya Air Force One siku ya Jumatatu, Trump alisema: “Hakuna mtu anayeniambia nini tunapaswa kuuza au tusiuze.”
Trump aliielezea Uturuki kuwa “mshirika mkubwa” wa Marekani na kusema imefanya kazi nzuri katika masuala ya kikanda, hususan nchini Syria.
Ingawa alikiri kwamba Uturuki si rafiki mkubwa wa Israel wala wa Netanyahu, Trump amesisitiza kuwa uhusiano kati ya Marekani na Uturuki unaendelea kuwa imara.
Katika mkutano wa NATO, Trump amesema angeweza “kuzingatia kwa umakini” kurejesha mauzo ya ndege za F-35 kwa Uturuki, akieleza kuwa Uturuki imeonyesha uaminifu mkubwa kuliko baadhi ya nchi nyingine washirika.
Mtazamo chanya
Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, alisema Trump ameonyesha “mtazamo chanya” kuhusu uwezekano wa kuiuzia Uturuki ndege hizo za kivita za F-35.
Kauli za Trump zimeunga mkono taarifa za awali za vyombo vya habari zilizodai kuwa alikuwa amekasirishwa na ukosoaji wa hadharani wa Netanyahu kuhusu mpango wa Marekani wa kuiuzia Uturuki ndege hizo.
Mwaka 2019, wakati wa muhula wa kwanza wa Trump madarakani, Marekani iliiondoa Uturuki katika mpango wa F-35 baada ya Uturuki kununua mfumo wa ulinzi wa makombora wa Urusi wa S-400. Washington imedai kuwa mfumo huo wa Urusi ungeweza kuhatarisha usalama wa teknolojia ya ndege za F-35.
Hata hivyo, Uturuki imekuwa ikisisitiza mara kwa mara kwamba hakuna mgongano kati ya mfumo wa S-400 na ndege za F-35, na ilipendekeza kuundwa kwa tume maalumu ya kuchunguza suala hilo.
Aidha, Uturuki inasema ilitimiza kikamilifu wajibu wake katika mpango wa F-35 na kwamba kuondolewa kwake kulikiuka makubaliano yaliyokuwepo. Pia inaamini kuwa kumiliki ndege hizo kutaimarisha si tu uwezo wa ulinzi wa Uturuki, bali pia nguvu za muungano wa NATO kwa ujumla.















