Vita vinavyoendelea kwa zaidi ya miaka mitatu kati ya jeshi la Sudan na kikosi cha RSF vimeharibu kwa kiasi kikubwa mfumo wa afya wa nchi hiyo.
Hili ni wimbi la tatu la maradhi ya kipindupindu nchini Sudan katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo, na lilianza wiki mbili tu baada ya mlipuko uliopita kutangazwa kumalizika mwezi Machi.
Kati ya Julai 2024 na Machi 2026, zaidi ya watu 124,400 waliambukizwa na 3,500 walifariki dunia wakati wa wimbi la mwisho, kulingana na takwimu za serikali.
Takriban watu 300 washukiwa kuathirika Kordofan Kaskazini
Msimu wa mvua nchini Sudan unatarajiwa kuongezeka katika wiki zijazo, ambapo maambukizi ya kipindupindu huongezeka kutokana na mamilioni ya watu kukosa maji safi, huku mvua zikizidi kuzuia upatikanaji wa misaada.
Serikali ya Sudan ilitangaza mlipuko huo mpya wiki hii katika jimbo la Kordofan Magharibi.
WHO ilisema mlipuko huo unaonekana kuendelea kusambaa, kufuatia ripoti za karibu kuambukizwa kwa takriban watu 300 huku watu watatu wakfariki dunia katika jimbo jirani la Kordofan Kaskazini, ambako Umoja wa Mataifa umeonya kuwa RSF inajiandaa kufanya mashambulizi makubwa ya ardhini dhidi ya mji mkuu wa jimbo la Al Obeid.
Mashambulizi ya ndege zisizo na rubani katika vituo vya umeme vya mji huo tayari “yanavuruga upatikanaji wa maji salama ya kunywa na umeme,” mkuu wa misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa Tom Fletcher alisema Jumanne, akionya kuhusu hatari ya mauaji ya halaiki.
Hospitali zilizoathirika
Baada ya miaka mitatu ya vita, karibu hospitali zote nchini humo zimelazimika kufungwa kabisa au kufanya kazi kwa sehemu tu.
“Asilimia 40 ya vituo vya afya havifanyi kazi kabisa, na karibu asilimia 60 iliyobaki vinafanya kazi kwa kiwango kidogo tu, maana yake vinatoa huduma chache au zisizotosha kwa wagonjwa wa eneo hilo,” alisema Dkt. Shible Sahbani ambaya ni Mwakilishi wa WHO nchini Sudan.















