Jumla ya wabunge 216 walipiga kura kuunga mkono muswada wa kuongeza muda wa rais kusalia madarakani, hivyo kuvuka kiwango cha kura 187 kilichohitajika ili kupata uungwaji mkono wa theluthi mbili ya wabunge.
Muswada huo sasa utapelekwa katika Bunge la Seneti, ambapo unatarajiwa pia kupitishwa kwa urahisi kutokana na chama tawala cha ZANU-PF kuwa na ushawishi mkubwa kupitia viongozi wa kimila na wawakilishi wengine ambao kwa kawaida hupiga kura sawa na chama hicho.
Dalili kwamba Mnangagwa mwenye umri wa miaka 83 alitaka kuendelea kubaki madarakani baada ya kumalizika kwa muhula wake wa pili mwaka 2028 zilianza kujitokeza takriban miaka miwili iliyopita, wakati wafuasi wake walipoanza kuimba nyimbo za kuashiria hilo katika mikutano ya ZANU-PF wakidai apewe muda zaidi wa kutekeleza ajenda yake.
Mwaka jana, chama hicho kiliazimia kubadilisha Katiba ili kuongeza muda wa mihula ya urais, na mpango huo ulipata idhini ya Baraza la Mawaziri mwezi Februari mwaka huu.
Wakosoaji wanasema muswada huo ni mbinu ya kumwezesha Mnangagwa kubaki madarakani kwa muda mrefu zaidi, huku wanaounga mkono wakidai kuwa utaimarisha uwajibikaji wa viongozi na kuleta utulivu wa kisiasa nchini.
Mnangagwa aliingia madarakani baada ya mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 2017 yaliyomuondoa madarakani Robert Mugabe, ambaye alikuwa ameiongoza Zimbabwe tangu ilipopata uhuru mwaka 1980.
Kabla ya kutofautiana kisiasa katika miezi iliyotangulia mapinduzi hayo, Mnangagwa alikuwa mmoja wa washirika wa karibu zaidi wa Mugabe na aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali za juu serikalini, ikiwemo nafasi ya makamu wa rais.
Baadhi ya wanaharakati na maveterani wa vita vya ukombozi vya Zimbabwe waliwasilisha kesi mahakamani kupinga mpango wa kuongeza muda wa Mnangagwa kama mkuu wa nchi, lakini kesi hizo ziliondolewa kwenye ratiba ya mahakama wiki hii kutokana na sababu za kiufundi.















