Waandamanaji wanaopinga kujengwa kwa kituo cha Marekani cha Ebola wakamatwa nchini Kenya

Ujenzi wa kituo cha Ebola ulizuiwa kwa muda na Mahakama ya Juu nchini Kenya na pia umekuwa ukipingwa na wanasiasa wa nchi hiyo.

Newstimehub

Newstimehub

9 Juni, 2026

67dd6fca16904dc721459fef10edbe40cb6ca545aae092a832bb698efb9b6a40

Wakenya kadhaa wamekamatwa Jumanne wakiwa katika maandamano ya kupinga ujenzi wa kituo cha Karantini cha Ebola kinachojengwa kwa ajili ya raia wa Marekani katika mji wa kitalii.

Kituo hicho, katika Kambi ya Jeshi la Anga ya Laikipia, mjini Nanyuki, katika eneo la Mlima Kenya, kitatumika kwa ajili ya karantini kwa raia wa Marekani wanaotoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, ambayo hivi sasa inakabiliwa na mlipuko wa Ebola.

Mpaka sasa, Kenya bado haina rekodi yoyote ya mgonjwa wa Ebola, na wengi wanapinga wazo la kuleta watu wanaoshukiwa kuwa na ugonjwa ambao unaambukiza kwa kasi nchini mwao.

Mamia walikusanyika katika eneo la kambi hiyo, wengine wakiwa wamevaa zana za kujikinga huku baadhi wakiwa wamebeba majeneza yaliyoandikwa “Ebola.”

‘Hatuna Ebola’

AFP imerekodi watu kadhaa waliokamatwa na polisi, ambao pia walirusha vilipuzi vya kutoa machozi kwa lengo la kutawanya vikundi vya watu.

Kituo hicho ambacho kimepangwa kuwa na vitanda 50 vilivyotengwa na kuendeshwa na wafanyakazi wa Marekani, kilifikia hatua za kukamilika mwishoni mwa juma.

Ujenzi ulisita baada ya Mahakama Kuu kuweka zuio la muda mfupi kufuatia malalamiko kutoka kwa wananchi na wanasiasa wa eneo hilo.

Hata hivyo, Rais William Ruto wa Kenya, serikali yake imesisitiza kuendelea na mpango huo, na kusema kuwa haitakuwa vyema kuikatalia Marekani ombi lake la kuweka kituo nchini humo.

Kwa nini Kenya ‘haiwezi kukataa’

“Watu wa Marekani na serikali wamekuwa washirika wetu wa muda mrefu katika masuala ya afya kwa takriban miaka 25-30,” amesema Rais Ruto wiki iliyopita.

“Itakuwa vibaya sana, iwapo ombi moja la Marekani la kuweka kituo kwa gharama zao, sisi tutakataa. Tutaonekana sio binadamu.”

Waziri wa Afya nchini Kenya amesisitiza kwamba, Wakenya pia watatumia kituo hicho.

Marekani imeahidi kiasi cha fedha Dola milioni 13.5 kama sehemu ya jitihada za kukabiliana na Ebola.

Hatua hii inafutia makubaliano tata yaliyofikiwa miaka miwili iliyopita, ambapo Kenya ilikubali kutoa taarifa zake za afya kwa Marekani ikiwa ni mbadala wa msaada wa fedha.

Shirika la Afya Duniani limetangaza hali ya dharura ya kimataifa kutokana na mlipuko wa Ebola nchini DRC, ambapo wagonjwa 515 wamethibitishwa, ikiwemo vifo 91.

Licha ya hofu ya kuenea katika nchi jirani, ni Uganda pekee iliyorekodi maambukizi.

Mpaka sasa, wagonjwa 19 wamethibitishwa, wote wakiwa ni raia wa DRC waliovuka mpaka.