Somalia na Qatar zimesaini makubaliano ya ushirikiano wa ulinzi yanayolenga kuimarisha uhusiano wa kijeshi na kupanua uratibu wa kiusalama kati ya nchi hizo mbili.
Makubaliano hayo yalisainiwa na Waziri wa Ulinzi wa Somalia, Ahmed Moalim Fiqi, na Waziri wa Ulinzi wa Qatar, Saud bin Abdulrahman bin Hassan Al Thani, pembeni mwa Maonesho ya Kimataifa ya Vifaavya Ulinzi wa Baharini jijini Doha, Qatar (DIMDEX), kwa mujibu wa Shirika la Habari la Serikali ya Somalia (SONNA).
Makubaliano hayo yanalenga kuimarisha ushirikiano wa kijeshi, kuanzisha na kuendeleza mifumo ya uratibu wa kiusalama, pamoja na kuunga mkono juhudi za pamoja za kudumisha usalama na utulivu katika ngazi ya kikanda na kimataifa, SONNA ilisema.
SONNA iliongeza kuwa makubaliano hayo yanaakisi kuimarika kwa ushirikiano wa kimkakati kati ya Jamhuri ya Shirikisho la Somalia na Dola ya Qatar, yakionyesha maslahi ya pamoja katika kupanua ushirikiano katika nyanja za ulinzi na usalama.
Siku ya Jumatatu 19, Januari 2026, Amir wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani, alizindua rasmi toleo la tisa la DIMDEX, linalofanyika katika Kituo cha Kitaifa cha Mikutano cha Qatar jijini Doha.
Tukio hilo la siku nne linawakutanisha zaidi ya makampuni 200 ya Qatar na ya kimataifa yanayojihusisha na sekta za ulinzi wa baharini, nchi kavu na anga.
Maonesho hayo pia yameshuhudia ushiriki mkubwa wa kihistoria kutoka kwa wajumbe wa ngazi za juu wa serikali, huku zaidi ya wajumbe 110 kutoka mataifa mbalimbali duniani wakihudhuria.









