Waziri wa Ulinzi wa Somalia, Ahmed Moallim Fiqi, amepongeza vikosi vya usalama vya nchi hiyo pamoja na wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika kwa kufanikisha kurejesha mji wa kimkakati wa Bariire kutoka kwa magaidi wa Al Shabab, akisema wameonyesha ”ushujaa na kujitolea.”
Jeshi la Kitaifa la Somalia (SNA), kwa kushirikiana na Jeshi la Ulinzi la Watu wa Uganda (UPDF) chini ya Mpango wa Mpito wa Umoja wa Afrika nchini Somalia (AUSSOM), walikomboa mji huo ulioko katika eneo la Lower Shabelle kutoka kwa magaidi wa Al Shabab baada ya siku kadhaa za operesheni za ardhini na angani.
Zaidi ya magaidi 100 wa Al Shabab waliuawa, kulingana na wizara ya ulinzi ya Somalia. Wizara hiyo iliongeza kuwa wanajeshi wawili wa Somalia waliuawa na wengine 12 walijeruhiwa katika mapambano hayo.
”Ningependa kupongeza ushujaa na ushindi wa vikosi vyetu vya mstari wa mbele hasa katika Bariire kwani wamekuwa wakipambana na magaidi wa Al Shabab kwa wiki nzima,” Waziri wa Ulinzi Fiqi alisema katika mkutano na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki.
Raia kurejea nyumbani
Alisema magaidi walikuwa wameweka vifaa vya milipuko, kuchimba mahandaki na kuzindua mashambulizi kadhaa ili kuzuia vikosi kusonga mbele katika mji huo. Hata hivyo, ”mbinu zao zimeshindwa,” Fiqi alisema.
”Al Shabab wamepata pigo kubwa ambapo takriban magaidi 120 waliangamizwa, zaidi ya 100 walijeruhiwa, na wengine wengi walikamatwa. Pia walitelekeza silaha zao,” Waziri wa Ulinzi wa Somalia alifichua.