Watu tisa wamefariki dunia na wengine 19 kujeruhiwa kufuatia tukio la mkanyagano lililotokea siku ya Jumatatu ndani ya hekalu moja nchini India.
Tukio hilo limetokea ndani ya hekalu la Ashok Dham liloloko katika wilaya ya Lakhisarai, wakati wakifanya ibada kwa mungu wa kihindu, maarufu kama Shiva.
Mkanyagano huo, ulianza baada ya kuzuka taarifa za kuanguka kwa nguzo ya umeme ndani ya hekalu hilo, hali iliyopelekea waamini hao kuanza kuhamaki na kuanza kukimbia.
Novemba mwaka jana, watu tisa walipoteza maisha baada ya mkanyagano ndani ya hekalu kusini mwa jimbo la Andhra Pradesh, nchini India.
Katika tukio lingine, watu 36 walifariki dunia mwaka jana, baada ya kukanyagana wakati wa mkutano wa siasa katika jimbo la Tamil Nadu nchini humo.















