Marekani imewawekea vikwazo wanaodaiwa kuwa viongozi wa kijasusi wa makundi mawili makubwa ya waasi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambako mapigano yamekuwa yakiendelea mashariki mwa nchi.
Vikwazo hivyo vinawalenga Gustave Kubwayo, anayedaiwa kuwa kamanda wa FDLR, na John Imani Nzenze, anayedaiwa kuwa kamanda wa M23 na mkuu wa ujasusi, Wizara ya Fedha ya Marekani ilisema katika taarifa siku ya Jumanne.
Eneo la mashariki la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo lenye utajiri mkubwa wa madini limekumbwa na machafuko kutoka kwa makundi mbalimbali yenye silaha kwa zaidi ya miongo mitatu.
Tangu 2021, M23 imedhibiti maeneo kadhaa na mapigano yameendelea tangu kuanza kwa mwaka 2025.
Marekani inasema imedhamiria kurudisha amani mashariki mwa DRC
Wiki iliopita, mapigano mengine yalianza kati ya vikosi vya serikali na waasi wa M23 eneo la Masisi, mkoa wa Kivu Kaskazini.
Katika taarifa, Waziri wa Fedha wa Marekani Scott Bessent amesema Rais Donald Trump “amekuwa wazi kuwa kuna haja ya kumaliza mzozo wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo mara moja, na Marekani imedhamiria kuleta amani na maendeleo katika eneo hilo.”
Aliongeza kuwa machafuko yanayoendelea “yanatatiza zaidi hali ambayo ni mbaya kwa watu na kuwa tishio kwa maslahi ya Marekani eneo hilo.”















