Makamu wa Rais wa Tanzania Deogratius Ndejembi, ametoa wiki mbili kwa Wizara ya Mipango, Kilimo na Fedha kuandaa mpango wa mafunzo kwa vitendo utakaowapa angalau vijana 10,000 fursa katika Taasisi na Mashirika ya Umma ya Kufanya mafunzo kwa Vitendo huku wengine 20,000 wakilengwa katika sekta binafsi.
Akizungumza Arusha wakati akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan kwenye ufunguzi wa Kikao Kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Mashirika ya Umma C-CEOs Forum 2026. Makamu wa Rais, amesema mpango huo utawajengea vijana uzoefu wa kuajirika na kujiajiri, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Dira 2050.
Aidha, ameyataka Mashirika ya Umma kuwa injini ya mageuzi ya uchumi, kuongeza tija, kubana matumizi yasiyo ya lazima na kuhakikisha uwekezaji wa Serikali unaleta matokeo yanayogusa maisha ya wananchi.















