Maandamano hayo yaliandaliwa na makundi ya ulinzi wa kiraia pamoja na mashirika ya kijamii, yakifanyika katika miji mikubwa ikiwemo Johannesburg, Pretoria, Durban na Cape Town.
Aidha, maandamano hayo yamefanyika baada ya kampeni iliyodumu kwa miezi kadhaa, ambapo waandaaji walitoa wito kwa wahamiaji wasio na vibali kuondoka nchini kabla ya Juni 30. Hatua hiyo imeibua hofu ya kurejea kwa mashambulizi ya chuki dhidi ya wageni.
Waandamanaji wanadai kuwa wahamiaji wanachukua nafasi za ajira kwa kukubali mishahara midogo katika taifa ambalo kiwango rasmi cha ukosefu wa ajira ni takriban asilimia 32. Pia wanawalaumu kwa kuongezeka kwa uhalifu, msongamano katika hospitali na shule za umma, pamoja na ushindani katika sekta isiyo rasmi ya biasharaMsitafute wa kulaumiwa
Msitafute wa kuwalaumu
Mapema mwezi huu, Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, aliwataka wananchi kutowalaumu wahamiaji kwa changamoto za kiuchumi na kijamii zinazoikabili nchi hiyo.
“Kutatua changamoto hizi kunahitaji suluhisho la vitendo, si kuwafanya watu walio katika mazingira magumu kuwa wa kulaumiwa,” alisema Ramaphosa katika taarifa yake.
Katika mji wa bandari wa Durban, waandamanaji waliovalia mavazi ya jadi ya Kizulu walipita mitaani wakiwa na fimbo na ngao huku wakiimba “abahambe,” neno la Kizulu linalomaanisha “waondoke.”
Mjini Cape Town, kundi la wanaharakati waliopinga maandamano hayo lilibeba mabango yaliyohimiza amani na kutotumia vurugu.
“Hakuna Mwafrika anayepaswa kufukuzwa barani Afrika”
Shaheed Mahomed wa kampeni ya Siyafuna Sonke Action alisema hakuna Mwafrika anayepaswa kuchukuliwa kuwa kinyume cha sheria akiwa barani Afrika.
“Hakuna Mwafrika anayepaswa kuchukuliwa kuwa kinyume cha sheria akiwa barani Afrika. Tunapaswa kuungana kama wafanyakazi wa Afrika,” alisema Mahomed.
Aliongeza kuwa wahamiaji wamekuwa sehemu ya historia ya mapambano ya Afrika Kusini kwa muda mrefu na akawahimiza wafanyakazi Weusi kutogeukiana, akidai kuwa adui wao halisi ni ubeberu na mfumo wa kibepari.
Katika jiji la Johannesburg, zaidi ya waandamanaji 4,000 walitembea kuelekea eneo la Hillbrow, ambalo lina idadi kubwa ya wahamiaji.
“Imetosha. Tumewavumilia kwa muda mrefu. Sasa ni wakati wao kurudi nyumbani – abahambe, waondoke,” alisema dereva wa teksi Malumee Yohanes.
Polisi waimarisha ulinzi
Idadi kubwa ya polisi ilisimamia maandamano hayo huku biashara nyingi katika kitovu cha biashara cha Johannesburg zikifungwa kutokana na hofu ya vurugu na uporaji.
Idadi halisi ya wahamiaji wasio na nyaraka nchini Afrika Kusini bado inabishaniwa, ingawa makundi yanayopinga uhamiaji yanakadiria kuwa zaidi ya watu milioni tatu wanaishi nchini humo bila vibali katika taifa lenye wakazi wapatao milioni 65.
Wahamiaji wengi hujipatia kipato kupitia sekta isiyo rasmi kwa kuendesha maduka, biashara za mitaani na biashara za nguo.
Hakuna vurugu zilizoripotiwa
Licha ya tahadhari zilizotolewa na makundi ya kutetea haki za binadamu kuhusu uwezekano wa kuzuka kwa mashambulizi mapya ya chuki dhidi ya wageni, polisi walieleza kuwa hadi Jumanne alasiri hakukuwa na taarifa za vurugu wala majeruhi.
Wahamiaji wengi nchini Afrika Kusini wanatoka mataifa mbalimbali ya Afrika na Asia, hususan Pakistan, India na Bangladesh, ingawa waliolengwa zaidi katika kampeni ya sasa ni Waafrika.
Kabla ya maandamano hayo, mamlaka zilikuwa zimepeleka mamia ya maafisa wa polisi kote nchini ili kuimarisha usalama.
Wakati huo huo, mataifa kadhaa ya Afrika, yakiwemo Ghana, Nigeria, Malawi, Zimbabwe na Msumbiji, tayari yameanza kuwarejesha raia wao kutokana na kuongezeka kwa mvutano.
Viongozi wa kampeni ya kupinga uhamiaji wanatarajiwa kuwasilisha orodha ya madai yao kwa maafisa wa serikali baadaye Jumanne.















