Waziri wa Ulinzi wa Marekani Pete Hegseth ametoa ujumbe wa video akiapa kupambana na juhudi za kumng’oa madarakani na kutetea vita vya Iran kama “jasiri na vya kihistoria” baada ya Makamu wa Rais JD Vance kusema iliwagharimu Warepublican udhibiti wa Bunge.
Matamshi ya Hegseth, yaliyochapishwa kwenye mitandao ya kijamii siku ya Alhamisi, yalikuja huku kejeli kutoka kwa maadui zake katika Bunge zikizidi na Rais Donald Trump akipuuza maswali kuhusu kama anaweza kumfukuza kazi Hegseth.
Trump amempongeza mkuu wake wa Pentagon.
Mbunge wa Chama cha Demokrasia katika Baraza la Wawakilishi, Hakeem Jeffries, aliuliza katika chapisho: “Kwa nini Pete Hegseth bado yupo?”
Hegseth, mtangazaji wa zamani wa Fox News, amekuwa mtu aliyeleta migongano ambaye amejitengenezea maadui hata ndani ya Chama chake cha Republican.
Wakosoaji katika Bunge wanalenga mwenendo wake wa vita vya Iran, ambavyo Makamu wa Rais JD Vance amesema viliwagharimu Warepublican udhibiti wa Bunge, kufukuzwa kwake maafisa wakuu wa jeshi na kuharibu uhusiano na wabunge huku utawala ukitaka kifurushi cha matumizi ya ulinzi cha dola trilioni 1.5.
Wademokrasia, walioshinda udhibiti wa Bunge katika uchaguzi wa Jumanne, wameahidi kumchunguza Hegseth na jinsi alivyoshughulikia Pentagon, na wasaidizi wa bunge wanasema hilo litajumuisha kufutwa kazi kwa mwenyekiti wa Wakuu wa Wafanyakazi, miongoni mwa masuala mengine.
Haitafanikiwa dhidi yangu — Hegseth
Mbunge wa chama cha Republican, Thomas Massie, ameahidi kuwasilisha tena hoja za kumshtaki Hegseth (ili kumwondoa madarakani) wiki ijayo, akionya kwamba mchakato huo utakuwa “wa upole zaidi” ikilinganishwa na yale yanayomsubiri pindi chama cha Republican kitakapokabidhi udhibiti wa Bunge kwa chama cha Democratic mwaka ujao.
“Watafanya vikao vya kusikiliza na kesi,” Massie aliandika kwenye mtandao wa X.
Hegseth alitetea utendaji wake katika Wizara ya Ulinzi (Pentagon) kupitia video iliyochukua zaidi ya dakika nne, ambapo alijivunia hatua zake za kuwafukuza kazi viongozi wa ngazi za juu wa Pentagon, kusitisha mipango ya kukuza utofauti (diversity initiatives), na kupiga marufuku watu waliobadili jinsia (transgender) kujiunga na jeshi.
“Unaona, wananishambulia — wanatushambulia — kwa sababu tunafanya kazi kwa ufanisi. Haitafanikiwa. Hatutarudi nyuma,” Hegseth alisema huku akizungumza mbele ya kamera.
Akielezea jaribio hilo la kumshtaki kama “la kitapeli” au “la uongo,” Hegseth alikumbusha kuwa Trump mwenyewe aliwahi kushtakiwa mara mbili.
“Yote haya ni siasa za kujaribu kuharibu sifa za mtu binafsi. Mbinu hii haikufanikiwa dhidi ya Rais Trump, na haitafanikiwa dhidi yangu. Hilo ni jambo la uhakika,” alisema.
Siku ya Alhamisi, Trump alimsifu Hegseth alipoulizwa kama anatarajia mabadiliko yoyote ya watumishi, akisema Waziri wake wa Ulinzi “amefanya kazi nzuri sana.” Trump alidokeza kuwa upinzani dhidi ya Hegseth unatokana na uamuzi wake wa kuwafukuza kazi majenerali.
“Tulikuwa na majenerali wengi sana. Kila mtu alikuwa jenerali wa nyota nne.”
“Sijawahi kuona kitu kama hicho. Na wengi wao walikuwa na itikadi za ‘woke’ (itikadi za kijamii zinazozingatia sana masuala ya utambulisho na haki za kijamii). Sipendi jenerali mwenye itikadi hizo. Hivyo, huenda ndiyo maana anakabiliwa na upinzani,” Trump aliwaambia waandishi wa habari katika Ofisi ya Rais (Oval Office).
Trump pia alisifu mchango wa Hegseth katika operesheni za kijeshi za Marekani nchini Venezuela na Iran. “Hali nchini Venezuela imekuwa ya kushangaza… na nchini Iran, tumekuwepo kwa miezi saba na tunadhibiti kila kitu ambacho tulitaka kukidhibiti,” alisema.
Hegseth yuko hatarini kuondolewa
Vyanzo vimesema Trump bado anaweza kumwondoa Hegseth wakati Warepublican wakitathmini hasara walizopata katika uchaguzi.
Siku ya Jumatano, Makamu wa Rais Vance alihoji hadharani kama vita dhidi ya Iran vilikuwa na tija, akisema vilisababisha Warepublican kupoteza udhibiti wa Bunge. Kauli hiyo isiyo ya kawaida iliibua maswali kuhusu iwapo Trump bado ana mpango wa kuendeleza operesheni kubwa za kijeshi dhidi ya Iran, jambo ambalo alikuwa ametoa tishio la kulifanya.
Mshauri mmoja wa Trump alisema Hegseth “yuko hatarini kuondolewa” kutokana na vita dhidi ya Iran.
Wizara ya Ulinzi imesema Hegseth “amejitolea kikamilifu” kuongoza Pentagon hadi mwisho wa muhula wa Trump.
Hegseth aliwasihi wabunge “wazalendo” kuidhinisha ombi la fedha linalolenga kuisaidia Pentagon kulipia gharama za vita dhidi ya Iran na vipaumbele vingine vya matumizi.
“Bila kujali mtazamo wa watu kuhusu vita hivi—ambavyo naamini ni juhudi za kishujaa na za kihistoria zitakazohakikisha Iran haipati kamwe silaha za nyuklia—tunahitaji kuendelea kujenga upya jeshi letu, kama Rais Trump alivyofanya katika muhula wake wa kwanza,” alisema Hegseth.
Seneta wa chama cha Republican, Thom Tillis, aliambia kituo cha habari cha CBS Jumanne usiku kwamba Hegseth “anakabiliwa na wakati mgumu wa kuwajibishwa,” na kwamba uhusiano wake mbaya na wabunge unadhoofisha juhudi za utawala wa Trump za kupitisha bajeti ya ulinzi ya dola trilioni 1.5 bungeni.
Hegseth pia anaweza kukabiliwa na uchunguzi mkali kutoka kwa Wanademokrats kuhusiana na sera yake kuhusu Ukraine, pamoja na mashambulizi ya kijeshi ya Marekani dhidi ya boti zinazoshukiwa kubeba dawa za kulevya katika maji ya Amerika ya Kusini—hatua ambayo baadhi ya Wanademokrats wanasema inaweza kuchukuliwa kama uhalifu wa kivita.
Mbunge Adam Smith, wa Chama Cha Demokrats anayetarajiwa kuongoza Kamati ya Huduma za Jeshi katika Baraza la Wawakilishi mwaka ujao, ameahidi kufanya usimamizi mkali katika masuala mbalimbali—kuanzia vita dhidi ya Iran hadi kile alichokiita mmomonyoko wa “msingi wa kutojiingiza katika siasa” ndani ya vikosi vya ulinzi.















