Rais wa Senegal, Bassirou Diomaye Faye, amepitisha muswada wa bajeti kutumia kura yake ya turufu, licha ya kukataliwa na bunge, hatua ambayo inaonekana kuwa muhimu katika kurejesha utulivu wa hali ya kifedha ya nchi hiyo, wakati Senegal ikiendelea na juhudi za kukidhi masharti ya kupata mkopo kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).
Ofisi ya rais ilisema katika taarifa iliyotolewa Alhamisi kwamba Faye “ameamua kuanza kutekeleza Muswada wa Bajeti ya mwaka 2026”, hatua iliyomwezesha kupitisha bajeti hiyo bila idhini ya Bunge.
Senegal, ambayo inakabiliwa na mzigo mkubwa wa madeni, imeingia katika mkwamo wa kisiasa na kibajeti ambao haujawahi kushuhudiwa. Rais Faye amekuwa katika mvutano na Bunge la Taifa, ambako chama cha upinzani cha Pastef chenye idadi kubwa ya wabunge kimekuwa kikikataa mapendekezo yake kuhusu bajeti.
Kiongozi wa chama cha Pastef, Ousmane Sonko, ambaye aliwahi kuwa mshirika wa karibu wa kisiasa wa rais lakini baadaye akageuka kuwa mpinzani wake, anapinga hatua ya kurekebisha madeni ya nchi, ambayo inahitajika katika masharti ya mkopo wa IMF.
Hapo awali, Sonko aliita mpango huo kuwa ni “aibu” ambayo ingeweza kuhatarisha uhuru wa Senegal katika kufanya maamuzi yake.
“Anakosea sana”
Ingawa chama cha Pastef bado hakijatoa tamko rasmi kuhusu uamuzi wa rais, mbunge mwenye ushawishi mkubwa wa chama hicho, Amadou Ba, aliandika kwenye mtandao wa Facebook kwamba rais “amefanya kosa kubwa” na kwamba “hana mamlaka ya kuanza kutekeleza muswada wa bajeti ambayo umekataliwa na Bunge”.
Mwezi Septemba, Senegal ilitangaza kuwa imefikia makubaliano na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kuhusu mpango wa ufadhili wa madeni wenye thamani ya Dola bilioni 2.2 za Marekani, unaolenga kuimarisha hali ya kifedha ya serikali.
Hata hivyo, bodi ya utendaji ya IMF bado haijatangaza kuidhinisha mpango huo, ambao utekelezaji wake unategemea kutimizwa kwa masharti kadhaa.
Bajeti iliyorekebishwa ya mwaka 2026 pamoja na rasimu ya muswada wa bajeti ya mwaka 2027 ni nyenzo muhimu katika kushughulikia deni kubwa la Senegal. Mpango wa mkopo wa IMF unalenga kusaidia kukabiliana na changamoto hiyo.
Kwa upande mwingine, uamuzi wa Faye umepokelewa kwa furaha na Cheikh Diop, kiongozi wa chama kikuu cha wafanyakazi nchini humo, CNTS-FC, ambaye amesema hatua hiyo imeleta “nafuu kubwa kwa sekta ya wafanyakazi”.
Kwa mujibu wa Diop, hatua hiyo itawezesha kulipa madeni ya ndani ambayo “yanaathiri sana maisha ya wafanyakazi, uchumi kwa ujumla, pamoja na sekta ya ujenzi na kazi za umma”.
Athari kwa uchumi
Serikali imeonya kuwa kushindwa kupitisha bajeti iliyorekebishwa kunaweza kuhatarisha upatikanaji wa umeme, ulipaji wa madeni inayodaiwa na makampuni pamoja na utoaji wa malimbikizo ya mishahara kwa walimu.
Uamuzi wa kuipitisha bajeti hiyo kupitia amri ya rais umefanyika wakati Bunge la Taifa likionekana kuwa tayari kuukataa muswada wa bajeti ya mwaka 2027 uliopendekezwa na serikali.
Baadhi ya vipengele vya muswada huo vilikataliwa na wabunge wakati wa kikao cha Bunge kilichofanyika Jumatano, baada ya kukataliwa kwa mapendekezo kama hayo katika kamati za Bunge wiki iliyotangulia.
Wiki iliyopita, IMF ilisema iko tayari kujadiliana na wadau mbalimbali nchini Senegal kuhusu masharti ya mpango wa kupunguza mzigo wa madeni, huku mkwamo wa kisiasa ukiendelea kutishia utekelezaji wa mpango huo.
Msemaji wa IMF, Julie Kozack, alisema katika mkutano na waandishi wa habari wakati huo kwamba hatua inayofuata ya mpango huo wa kupunguza madeni “inategemea kukamilishwa kwa hatua zilizokubaliwa kuhusu mfumo wa bajeti”.
Senegal ilikabiliwa na deni la sekta ya umma lililokadiriwa kufikia asilimia 132 ya pato la taifa (GDP) mwishoni mwa mwaka 2024.















