Tigray People’s Liberation Front (TPLF), waasi wa kaskazini mwa Ethiopia, wamedhibiti uwanja wa ndege katika mji mkuu wa kanda hiyo, vyanzo vya kiusalama na eneo hilo viliiambia AFP siku ya Jumatano.
TPLF, ambao wanadhibiti kanda hiyo, walipigana katika vita vya wenyewe kwa wenyewe na serikali kuu mwaka 2020-2022 vilivyosababisha vifo vya watu karibu 600,000, kulingana na makadirio ya Umoja wa Afrika.
“Tulipokuwa njiani kwenda uwanja wa ndege kwa kazi, meneja wetu alimpigia dereva simu na kumwambia kuwa uwanja wa ndege umedhibitiwa na vikosi vya Tigray. Kwa kuwa hakukuwa na ndege, alituambia turudi nyumbani,” mfanyakazi wa kampuni ya Alula Aba Nega katika mji mkuu wa mkoa wa Tigray, Mekelle aliiambia AFP.
Taarifa hizo zilithibitishwa na chanzo kimoja cha usalama wa taifa la kigeni nchini Ethiopia.
‘Ndege hazipai’
Idadi ndogo ya polisi wa serikali kuu wanalinda uwanja huo wa ndege, na hali yao haikuwa inajulikana.
Rada za ndege, na ufuatiliaji, zilionesha ndege ya Jumatano asubuhi kutoka Mekelle na mji mkuu, Addis Ababa, haikuweza kuondoka.
“Shirika la Ethiopian Airlines limesitisha safari zake za kwenda Mekele, Axum, na Shire kuanzia leo, kutokana na hali ilivyo sasa kanda ya Tigray,” shirika hilo la taifa lilisema kwenye taarifa.
Ethiopia inakabiliwa na changamoto nyingi za kiusalama, ikiwemo katika kanda zake zenye idadi kubwa ya watu, Oromia na Amhara.















